WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema ujenzi wa Daraja jipya la Selander lililopo jijini Dar es Salaam lenye urefu wa km. 1.03 na upana wa mita 20.5 ujenzi wake umefikia asilimia 93, kwamba linatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu.
Daraja hilo lenye barabara unganishi zenye urefu wa km 5.2 linajengwa na Kampuni ya GS Engineering ya Korea, litakalopita baharini kuanzia ufukwe wa Coco Beach (Oysterbay) kwenda Hospitali ya Aga Khan (Maeneo ya Ocean Road).
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo, Waziri Mbarawa alisema hadi sasa mradi huo umefikia asilimia 93 na kwa sasa mkandarasi anaendelea na ujenzi wa sehemu ya juu ya daraja baada ya kukamilisha ujenzi wa sehenu ya chini kwa asilimia 100 ikiwamo, nguzo za msingi 254, vitako vyake 16 pamoja na nguzo 16 za juu za daraja.
“Mkandarasi amekamilisha kujenga km 1.026 kati ya km 1.030 sawa na asilimia 99.7 na kuweka nyaya za daraja 30 kati ya 30 sawa na asilimia 100,” alisema Prof. Mbarawa.