Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Jokate Mwegelo ameagiza kuwekwa chini ya ulinzi kwa Viongozi wa Chuo cha Lubando Training College kilichopo Mtaa wa Butiama, Kata ya Mtoni Kijichi baada ya kubaini Chuo hicho kinaendeshwa kinyume cha Sheria.
DC Jokate ametoa agizo hilo wakati alipoungana na Wataalamu katika ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali ya Wilaya hiyo ambapo aliambatana pia na Mkurugenzi-Uthibiti, Ufuatiliaji na Tathmini kutoka NACTE Dkt. Joefrey Oleke.
Baada ya kufanya mahojiano na Mkuu wa Chuo hicho, DC Jokate alibaini kuwa kwa muda sasa Chuo hicho kimekua kikitoa mafunzo bila kupata usajili, pamoja na kutoa mafunzo kwenye mazingira yasiyo rasmi .
"Hamna kitu kibaya kama kufanya utapeli halafu ukadhani hutagundulika, Serikali ina macho kila sehemu, NACTE kaeni hapa na Polisi, lazima tupate 'information', Chuo hakijasajiliwa lakini hata mandhari yake haistahili, kuna Watu wanatoa huduma ambazo kiuhalisia hawastahili kutoa, tushirikiane katika ufuatiliaji, hawa wachukuliwe hatua kali huu ni utapeli -DC Jokate
Kwa upande wake Dkt. Jofrey Oleke amesitisha shughuli zote zinazoendelea katika chuo hicho, huku akielekeza taratibu nyingine za kisheria kufuatwa huku akisema kwa ukaguzi uliofanyika, chuo hicho hakitambuliki NACTE wala VETA.