Gekul Atoa Ufafanuzi Maslahi ya Wanaoshiriki VIDEO za Muziki "VIDEO MODEL"




Serikali imesema walimbwende, wachezaji, waigizaji, wanamitindo na watu wengine maarufu ambao hushiriki kwenye Sanaa katika video za wanamuziki kwa lengo la kuiongezea mvuto kazi husika wanafanya kazi kama watu wengine na wanastahili kusimamiwa maslahi na haki zao.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul Septemba 02, 2021 Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali Namba 36 la Mhe. Asia Abdulkarim Halamga, Mbunge wa Viti Maalum alilouliza juu ya mpango wa kuwatambua na kulinda maslahi ya Vijana waliojiajiri katika Sanaa ya burudani kama walimbwende.

“Sanaa hii imekuwa ikihitaji ushiriki wa Video Vixen na Video Kings, Serikali ilifanya marekebisho ya Sheria kifungu cha 47(b) mwaka 2019 ili kuipa COSOTA mamlaka ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mikataba ya kimaslahi kati ya wenye kazi hiyo ya Sanaa na Vijana wetu wa Video Vixen na Video Kings ili waweze kupata haki zao za kimkataba” amesema Naibu Waziri Gekul.

Aidha, Mhe. Gekul ameongeza kuwa watu hao hushirikishwa na wamiliki wa kazi husika kwa makubaliano maalumu katika kazi wanazofanya ili kuweza kuifikia na kuivutia hadhira yao.

Kwa mujibu wa Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki Na. 7 ya mwaka 1999, anaepaswa kulipwa mrabaha wa kazi ya sanaa ni mtunzi, mbunifu na mtayarishaji wa kazi ya Sanaa husika.

Pia Mhe. Gekul ametoa rai kwa wadau wote wa Sanaa ya Burudani kuishirikisha Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA) ili maslahi yao yaweze kulindwa kupitia mikataba.

Taasisi ya COSOTA) ni chombo cha kisheria kilichoanzishwa na Serikali ambayo ipo chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mujibu wa Sehemu ya 46 ya sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki Na. 7 ya mwaka 1999 kusimamia sheria hiyo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad