KATIKA kuhakikisha Yanga wanafanya vyema katika michuano ya kimataifa, uongozi wa timu hiyo kwa kushirikiana na wadhamini wao Kampuni ya GSM umeanza mipango mapema kwa kuweka mzigo wa maana ambao utaongeza hamasa ya ushindi kuelekea katika mchezo wao dhidi ya Rivers United ya nchini Nigeria.
Yanga Septemba 12, watakuwa na kibarua kizito cha kumenyana na Rivers United katika mchezo wa hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaofanyika katika Uwanja wa Mkapa, Dar.
Chanzo cha ndani kutoka Yanga kimeliambia Championi Jumamosi kuwa uongozi huo umeweka wazi mpango wa kuweka fedha za kutosha kwa ajili ya kuhamasisha ushindi kwa wachezaji kuelekea katika mchezo wao dhidi ya Rivers, jambo ambalo wanaamini litaongeza chachu ya ushindi kama ambavyo wamekuwa wakifanya katika michezo mingine mikubwa ya timu hiyo.
“Kama ambavyo imekuwa siku zote, siyo jambo geni kwetu ndani ya Yanga, imekuwa kawaida kwetu kuweka fedha kama motisha kwa wachezaji katika michezo mikubwa ili kuhamasisha ushindi.
“Hivyo hata katika mchezo wetu wa kimataifa dhidi ya wapinzani wetu Rivers itawekwa fedha ya kutosha ikiwa kama sehemu ya motisha kwa wachezaji na benchi la ufundi.
“Wadhamini wetu wakiongozwa na GSM wamekuwa wakisimamia hilo mara kwa mara kuhakikisha tunafanya vyema na tayari, tunawashukuru kwani malengo yamekuwa ni kufika katika hatua nzuri katika michuano hii ya kimataifa na sio kushiriki tu.
“Lazima kuwe na mambo mengi ya kuweka hamasa ndani ya timu na hivyo ndio hufanywa na klabu nyingi za kisasa kutoa bonasi za ushindi kwa timu pindi inapopata ushindi,” kilisema chanzo hicho.
Championi Jumamosi lilipomtafuta, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela kuhusu kuwekwa kwa ahadi ya fedha kuelekea katika mchezo huo alisema: “Bado ni mapema sana kuzungumzia suala la bonasi za mchezo huo hivyo kama kutakuwa au hazitakuepo mtafahamu huko mbeleni lakini kwa sasa bado ni mapema kusema,” alisema kiongozi huyo.
MARCO MZUMBE, Dar es Salaam
OPEN IN BROWSER