JINA la Irene Paul siyo geni kunako fani ya uigizaji Bongo almaarufu Bongo Movies. Mwanadada huyu ana sifa za kuwa mwigizaji hodari.
Ameshiriki filamu na vipindi kadhaa na kwa sasa anatisha kwenye Tamthiliya ya Jua Kali.
Kabla ya hapo amefanya vizuri mno kupitia filamu kama Love & Power, Kibajaji, Kalunde, Fikra Zangu, Penzi la Giza, I Hate My Birthday na nyingine kibao.
Waongozaji wengi wa filamu wanasema Irene anajua kuzitendea haki nafasi anazopewa kuigiza.
Ukimuuliza Irene kama yeye ni maarufu atakujibu;
“Sitaki kusema kuwa nina umaarufu mkubwa, ila ninachoweza kusema ni kuwa kazi zangu zinatambulika mno, hasa kwa kuwa ninafanya kazi na televisheni, basi mtu atajulikana kwa haraka kuliko kazi nyingine.
Uigizaji ambao amefaulu kuufanya kwenye filamu za Tanzania ni kwa kipindi cha miaka 11. Muda huu Irene anasema ameutumia kujitafutia nafasi ambazo zinasongesha taaluma yake kuwa juu zaidi.
Irene alianza kwa kuwa mtangazaji kwa miaka kadhaa kabla ya kujikita kwenye uigizaji.
Kipindi hiki ni cha tamthilia ambayo mwanadada huyu anaigiza kama mama wa kambo katika familia yenye baba mzee aliye na watoto ambao mmojawao ana umri sawa na wa mama wa kambo.
Tamthiliya hiyo imelenga kuangazia hali zinazofanyika kwenye baadhi ya ndoa barani Afrika ambapo katika ndoa yake kwenye tamhiliya, Irene anasema kuwa kuna vituko na vitimbi vya kila aina vinavyofanyika.
“Kwa mfano ninapopewa nafasi ya kuigiza kama mwanamke aliyesalitiwa kwenye ndoa, ninaweza kuwa simo kwenye ndoa, lakini kwa sababu mimi ni mwanamke aliyesalitiwa huwa tu ninaleta hisia zilizotokea baada ya kusalitiwa hivyo ninaweza kuigiza kwenye nafasi hizo,” anasema.
Kuhusu historia yake, Irene anasema amezaliwa na kusomea Tanzania. Akiwa mtoto mdogo alikuwa amefahamu kwamba alipenda kupigwa picha na pia akiwa shuleni alipendelea masomo yaliyokuwa yanaegemea sanaa na mawasiliano.
Kwa wakati mmoja alitamani kuwa mwanahabari katika utu uzima kwa sababu alipenda ulimwengu wa kuonekana kwenye televisheni.
Anasema kuwa, alikuzwa katika hali hiyo hadi akasomea mafunzo ya uanahabari.
Pia anasema kwamba alikuwa anatamani kuwa mtangazaji, lakini watu wengi walimshauri kuwa anafaa zaidi kwenye uigizaji, hatua iliyomshinikiza kujitosa kwenye fani hiyo.
Irene anasema kuwa, kwa mtoto wa kike kuingia kwenye fani hiyo ilikuwa ni kama kupita kwenye ukuta.
Anasema alipitia changamoto chungu nzima ili kupata fursa alioynanayo kwa sasa. Anakiri kuwa alikuwa na muonekano tofauti na vigezo vilivyoakuwa vikiangaziwa miongoni mwa waigizaji.
Kwa mfano anasema kuwa alikuwa amenenepa kupitia kiasi na uso wake ulikuwa umejaa chunusi za kawaida wanawake wanapofikisha umri huo.
“Kusema kweli sikuwa mrembo, sikuwa na urembo ambao walikuwa wanatarajia, unajua katika viwango vyao vya urembo kwa mwanamke. Muigizaji, kuna kipindi Tanzania ikiwa haukutajwa kama Miss Tanzania au mlimbwende nafasi za kuigiza ulikuwa hupati.” Anasema Irene.
Anasimulia kuwa alipitia kipindi kimoja kizito cha kutafuta nafasi za uigizaji, kisa kimoja kingali akilini mwake alipotembea hadi sehemu moja ambapo utafutaji wa waigizaji ulikuwa unafanyika.
Alipofika mbele ya jopo lililopatiwa kazi hiyo anakumbuka maneno ya jaji mmoja yaliomuwacha na hisia chungu nzima.
“Aliniuliza kwani wewe unajionaje? Nikamjibu naweza kuigiza hapohapo akanitajia zaidi ya wanadada kama kumi hivi waliokuwa walimbwende Tanzania wakati huo, hata mimi nikashangaa, akaniambia kuwa akichagua mmoja kati ya walimbwende hao atakuwa bado na salio la wengine wazuri kisha akaniuliza hebu tuambie tumtoe nani hapo tukuweke wewe?
“Hapo niliishiwa na nguvu na kuona kweli sina nafasi tena.”
Irene anasema hakukata tamaa, alikubali kuchukua fursa za uigizaji bila malipo na pia nafasi ndogondogo ambazo zingesaidia kumkuza na kumwezesha kuendelea na azma yake ya kutaka kuwa muigizaji bora.
Anasema kuwa, mmoja wa watu waliokuwa kwenye jopo lililomkataa wakati mmoja alikuwa miongoni mwa watu waliomchagua miaka kadhaa baadaye kuigiza kwenye filamu mbili.
Ni ajabu kwamba, Irene anasema kuwa, miaka kadhaa baadaye alishiriki filamu hata na waigizaji kutoka nje ya nchi. Kilichomkuza zaidi kwao ni kuwa ana uwezo wa kuigiza kwa lugha ya Kingereza. Kuanzia wakati huo Irene anasema kuwa, alianza kunawiri na kutambulika kama mwigizaji.
Irene ameolewa na anasema kuwa imekuwa rahisi kudumisha ndoa yake kwa sababu alikutana na mume wake wakati ambapo alikuwa katika pilikapilika za kutafuta fursa hadi kufikia wakati huu ambapo ni mwigizaji mwenye jina.
Anamsifu mumewe kuwa miongoni mwa watu wanaomuunga mkono katika kazi yake.
Irene anasema kuwa anahisi kanakwamba wanawake bado hawajakubalika hasa wanapokuwa kwenye taaluma mbalimbali na hilo linadhihirika wazi kupitia yale aliyopitia.
Anasema uigizaji haufai kuchukuliwa kama dampo la kila aina ya watu kutupwa ndani yake kulingana na muonekano wao na maumbile yao mazuri, bali iwe na watu ambao wana elimu na maadili.
MAKALA: ELVAN STAMBULI