Huwezi Amini.. Achinjwa Kisa Deni la Tsh 400,000




MKAZI wa Majengo Sokola, katika Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, Gongo Charles (30), ameuawa kwa kuchinjwa na watu wanaodaiwa kumdai Sh. 400,000. Kwa mujibu wa baba mzazi wa marehemu, Charles Kwilasa, tukio la kuuawa mwanawe limetokea Agosti 4, mwaka huu, usiku.


“Majira ya saa mbili usiku tulipomaliza kula chakula familia nzima tukaingia kulala akiwamo marehemu, kumbe kijana wangu baadaye alitoka nje na baada ya kufika saa tano akaja kwenye dirisha la nyuma kumgongea mdogo wake,” alisema.


Kwilasa alisema, mdogo wake wakati anamfungulia kaka yake alikuwa na watu wawili na alipoingia ndani walianza kudaiana pesa.


Aliwanukuu wakisema; “tupe sasa hela zetu tuondoke”. Alisema kwa kuwa hakuwa na chochote aliingia chumbani kwenda kumwomba mdogo wake ambaye naye alimweleza hana kiasi chochote bali kiasi alichokuwa nacho tayari amenunua mchele.


Mzazi huyo aliendelea kusimulia kuwa vurugu zilianzia hapo wakati yeye hakujua kinachoendelea, lakini baada ya kusikia mwanawe akilia ndipo alipofungua mlango wake na kutoka nje na alikutana na watu wawili wakitoka nje haraka.


Aliendelea kusimulia kuwa kabla ya kuwafuatilia alifika mdogo wake na kumweleza kuwa kaka yake amepigwa na kucharangwa mapanga na watu wawili.


Kwa mujibu wa maelezo ya mzazi huyo wauaji baada ya kukosa kiasi wanachotaka na kabla ya kutekeleza mauaji hayo walimtaka marehemu akaombe kiasi hicho kwa baba yake.


Alisema hata hivyo, alikataa na kuwaahidi kuwa angewalipa baadaye ndipo watu hao walipopandwa na hasira na kumfanyia ukatili huo.


Mdogo wa marehemu, Derick Charles, alidai kuwa majira ya saa tano usiku aligongewa dirisha na kaka yake na alipokwenda kufungua mlango alirudi kulala, lakini baada ya muda mfupi kaka yake alimfuata chumbani na kumwomba kiasi cha Sh. 400,000 ili awakabidhi watu wawili aliofika nao ndani kwa madai kuwa wanamdai.


“Mimi nilimwambia kaka kwa sasa sina hela bali nimezinunua mchele kwa ajili ya kuuza kwenye kibanda changu baada ya kumweleza hivyo alirudi sebuleni na kulala.”


Alisema alimwambia kaka yake ambaye kwa sasa ni marehemu azime taa na kufunga mlango, lakini hakumjibu chochote. Muda mfupi baadaye alisema akasikia kelele za kuomba msaada na alipotoka chumbani alikuta akiwa ashafariki kwa kuchinjwa na kucharangwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake,” alisema Derick.


Derick alisema baada ya kushuhudia mauaji hayo wauaji walitokomea kusikiojulikana na aliamua kutoka nje ili kumweleza baba yake jinsi tukio lilivyotokea.


Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, George Kyando, alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kuongeza kuwa wanaendelea na msako ili kuwabaini watu waliofanya unyama huo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad