WAKATI viongozi wa Simba na wanachama pamoja na wadau mbalimbali wakiaga mwili wa aliyekuwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Zacharia Hans Poppe katika viwanja vya Karimjee, Mkurugenzi Mohammed Dewji hakuwepo.
Mmoja wa wajumbe wa Bodi hiyo, Cresentius Magori ametaja sababu ya Mo Dewji kutokuwepo ni kuwa yupo nje ya nchi na ametuma salamu za pole.
Magori ambaye pia ni mshauri wa Mo Dewji ameyasema hayo wakati akimzungumzia Hans Poppe ambaye amefanya naye kazi katika klabu hiyo.
Kupitia mtandao wa Instagram Mo Dewji baada ya kifo cha Hans Poppe kilichotokea Septemba 10 aliandika namna anavyomfahamu kiongozi huyo.
“Moyo wangu una maumivu makali sana. Bado ni vigumu kuamini na kukubali kuwa mjumbe wetu, kaka yetu, Zacharia Hans Poppe hatunaye tena,”
“Kaka yangu, nimefanya kazi na wewe kwa miaka mingi, na kila siku uliweka maslahi ya Simba mbele. Kaka yangu ulikua na wema wa kipekee, na ulikua wa kwanza na ulinyooka linapokuja suala la kuilinda Simba, hukuwa na maslahi binafsi. Ulikua rafiki wa marafiki wa Simba, na ulikua tofauti na wasioitakia mema Simba,”
“Kaka yangu, Umetangulia nasi tutafuata. Nitakukumbuka sana kaka yangu. Natoa pole sana kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki, pamoja na wanafamilia wote na mashabiki wa Simba kwa kumpoteza ndugu yetu. Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi,”
Hans Poppe anaagwa leo Dar na atazikwa Jumatano Mkoani Iringa, huku akiacha Simanzi kubwa kwa Wanasimba na wadau wa Michezo.