KOCHA Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze, amesema ametua kikosini hapo kuipa mataji, huku akisisitiza atashirikiana kikamilifu na kocha mkuu, Nasreddine Nabi.
Kaze amewahi kuwa Kocha Mkuu wa Yanga msimu uliopita ambapo alifanikiwa kuipa Kombe la Mapinduzi kabla ya kusitishiwa mkataba wake na nafasi yake kuchukuliwa na Nabi.
Akizungumza na Spoti Xtra, Kaze alisema: “Ninafuraha kubwa kuona nimerudi ndani ya Yanga nikiwa kama kocha msaidizi, hivyo malengo ya timu ndio malengo yangu pia, nipo katika sehemu ya malengo ya timu ambayo ni kuhakikisha tunatwaa ubingwa wa ligi kuu.
“Hivyo nikishirikiana na Kocha Mkuu, Nabi naamini malengo yatafanikiwa japo hakuna safari ambayo haina mabonde na milima, tutapambana kuhakikisha changamoto zote tunazitatua ili tufanikiwe.”
Wakati Kaze akisema hivyo, Kocha wa Viungo wa Yanga, Helmi Gueldich, ametamba kuwa wana matumaini makubwa kikosi chao kitakuwa tishio zaidi msimu huu.
“Tumefanya usajili bora kwa ajili ya msimu huu, lakini pia tuna benchi bora la ufundi hasa baada ya kuwepo maboresho kwa kuongeza baadhi ya wakufunzi akiwemo Kaze na Zahera (Mwinyi), tuna matumaini ya kuwa na kikosi tishio zaidi,” alisema.
PICHA: MUSA MATEJA