Dar es Salaam. Upande wa utetezi katika kesi ya kughushi inayowakabili viongozi watatu wa klabu ya Simba wameomba mahakama ya hakimu mkazi Kisutu kuahirisha kesi hiyo kutokana na kifo cha Zacharia Hans Poppe aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo iliyochukua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara nne mfululizo.
Amefariki dunia Septemba 10, 2021 katika hospitali ya Aga Khan alikokuwa akipatiwa matibabu na mazishi yake yanatarajiwa kufanyika kesho Septemba 15 mkoani Iringa.
Katika kesi hiyo Hans Pope na wenzake wawili, aliyekuwa rais wa klabu hiyo, Evans Aveva na makamu wake, Godfrey Nyange maarufu Kaburu, wanakabiliwa na mashtaka nane yakiweno ya kughushi, matumizi mabaya ya madaraka kwa kuhamisha fedha bila kamati ya utendaji ya Simba kukaa kikao.
Wakili wa washtakiwa hao, Benedict Ishabakaki na Kung'e Wabeya wametoa taarifa hiyo leo Jumanne Septemba 14, 2021 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya Aveva kuendelea kujitetea baada ya mahakama hiyo kuwakuta na kesi ya kujibu washtakiwa wote.
Mbali na kuomba mahakama hiyo iahirishwe shauri hilo, pia wamedai tarehe ijayo watawasilisha taarifa rasmi ya msiba wa HansPope ikiwemo cheti cha kifo.
Hakimu mkazi mkuu anayesikiliza shauri hilo, Thomas Simba amekubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Septemba 22, 2021 kupisha shughuli za mazishi.
Awali, wakili wa Serikali mwandamizi, Maghela Ndimbo aliieleza mahakama hiyo kuwa shauri hilo limeitwa mahakamani hapo kwa ajili ya washtakiwa kujitetea.
Kutokana na sababu zilizotolewa mawakili wa washtakiwa, Ndimbo ameiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea na kesi hiyo.
Agosti 31, 2021 kesi hiyo ilikwama kuendelea kutokana na HansPope kuwa mgonjwa na kushindwa kufika mahakamani hapo kuhudhuria kesi yake.
Imeandikwa na Hadija Jumanne na Irene Meena, Mwananchi