Dodoma. Spika wa Bunge, Job Ndugai ametishia kuifumua Kamati ya Bunge ya Bajeti baada ya kukerwa na kupitishwa kwa sheria inayoruhusu Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) kuanza kutoza ushuru wa bidhaa wa asilimia mbili kwa mazao nchini.
Spika Ndugai ameyasema hayo leo Jumatatu Septemba 6, 2021 bungeni mara baada ya majibu ya Wizara ya Kilimo yaliyotokana na swali la nyongeza la Mbunge wa Namtumbo (CCM), Vita Kawawa.
Kawawa amesema wakulima wa tumbaku wamekuwa wanalipa ushuru wa wilaya wa mazao, tozo ya vyama vikuu vya ushirika, chama cha msingi.
Amehoji kama ni kweli kuwa TRA mwaka huu itaanza kuwatoza wakulima wa tumbaku ushuru wa bidhaa.
Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema ni kweli Bunge lilipitisha sheria ya ushuru wa bidhaa wa asilimia mbili kwenye mazao ya kilimo.
Hata hivyo, amesema bado wizara haijaanza kukata ushuru huo kwasababu mjengeko wa bei ya tumbaku huamuliwa kati ya Februari hadi Aprili.
Amesema wakati sheria hiyo inapitishwa tayari mjengeko wa bei wa zao hilo ulikuwa umeshapitishwa.
Hata hivyo, amesema wizara yake imewasiliana na Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuwaandikia ili kuona namna gani watatekeleza sheria hiyo lakini kwa kulinda maslahi ya wakulima wa zao hilo.
Ndugai amesema wajumbe wa bajeti wanapaswa kuwa makini sana katika kazi zao kwasababu mambo yakifika bungeni wanaiamini kamati.
“Mkiendelea hivi nitaifumua hiyo, kamati ya bajeti tumeweka watu tunaowaamini sana. Sasa kama mnaenda kule mnalala tu na kupitisha tu vitu vya kienyeji mnatuponza. mnapitishaje kitu kama hiyo bwana,”amesema.