MMEKWISHA! Ndivyo utakavyoweza kusema ni baada ya Kocha Mkuu wa Simba, Mfaransa Didier Gomes kupata vikosi viwili matata katika kuelekea msimu ujao huku kikosi cha tatu pia kikiwa na uwezo wa kucheza na kupata matokeo dhidi ya timu yoyote.
Simba, leo Jumapili hii watashuka uwanjani kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo katika tamasha kubwa la Simba. Timu hiyo mara baada ya mchezo huo watajitupa tena kwenye Uwanja wa Mkapa Septemba 25, mwaka huu kuvaana na Yanga katika mchezo wa Ngao ya Jamii.
Mmoja wa viongozi wa Benchi la Ufundi la timu hiyo, ameliambia Championi kuwa kocha Gomes tayari ameshatengeneza muunganiko wa timu sambamba na kutengeneza vikosi vitatu atakavyovitumia katika msimu ujao na kwa kuanzia ataanza kukitumia kikosi cha kwanza katika mchezo wa kirafiki dhidi ya TP Mazembe, baadaye Yanga. Alikitaja kikosi cha kwanza kitatumia mfumo wa 3-5-2 kitakachokuwa hivi; kipa Aishi Manula, mabeki wa kati watatu ni Pascal Wawa, Enock Baka na Joash Onyango, viungo wa kati watano ambao ni Taddeo Lwanga, Sadio Kanoute, Rally Bwalya, Ousmane Sakho watakaocheza pamoja na Chris Mugalu.
Mawinga wa pembeni wawili akiwatumia Shomari Kapombe na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’. Kile cha pili kitatumia mfumo wa 4-4-2 ambacho nacho kitakuwa hivi, kipa Benno Kakolanya, mabeki wanne ni Israel Mwenda, Gadiel Michael, Pascal Wawa na Kennedy Juma, viungo ni Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Bernard Morrison na Duncan Nyoni, na mastraika wawili John Bocco na Denis Kibu.
Kikosi cha tatu ambacho ni 4-3-3; Jeremiah Kisubi, Kapombe, Tshabalala, Erasto Nyoni na Onyango, viungo Abdulsamad Kassim, Lwanga, Jimson Mwanuke, Hassan Dilunga, Yusuf Mhilu na Meddie Kagere.
Akizungumzia hilo, Kaimu Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema: “Hizo ni siri za kambi ngumu kuziweka wazi, kocha wetu anaendelea kukiboresha kikosi chetu kwa siri kwa lengo la kufanya vizuri katika msimu ujao.
“Kikubwa mashabiki wajitokeze kwa wingi katika Simba Day Jumapili kwa kujionea ubora wa kikosi chetu na mifumo hiyo atakayoitumia wakati kikosi chetu kikiwa uwanjani kikivaana na Mazembe,” alisema Kamwaga.