Maajabu.. Mama Ajifungua Mtoto Mzee, Madaktari Wafunguka




YAMKINI umepata kusikia mama aliyejifungua jiwe mkoani Mara katika Nchi ya Tanzania au mama aliyejifungua kiumbe wa ajabu na kusababisha taharuki kubwa, lakini simulizi inayozungumzwa zaidi kwa sasa ni ya mama aliyejifungua mtoto aliyezeeka na kuonekana kama bibi kizee wa miaka 70 na kuendelea, IJUMAA WIKIENDA linaripoti.


Katika hali isiyo ya kawaida mama mmoja raia wa Afrika Kusini mwenye umri wa miaka 20, amejifungua mtoto wa kike mwenye sura iliyozeeka au inayofanana na mtu mwenye umri uliofikia uzee huku akiwa katika hali kama vichanga wengine.


TAHARUKI
Mama huyo kutoka eneo la Libode ambako ni Mashariki mwa Jiji la Cape Town nchini Afrika Kusini, alijifungua mtoto huyo akiwa nyumbani hivi karibuni na kusababisha taharuki kubwa kwa watu wa jamii yake.



Kwa mujibu wa vyombo tofauti vya habari nchini Afrika Kusini, mama wa mwanamke huyo aliyejifungua mtoto huyo anasema kuwa, baada ya kuwa wamekosa gari la dharura ili kumuwahisha hospitalini baada ya kushikwa na uchungu mama huyo, waliamua ajifungulie nyumbani ambapo walishikwa na mshangao mkubwa kutokana na muonekano wa kichanga huyo.


TUKIO LA KUSHTUSHA
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya kimataifa nchini humo, tukio hilo linatajwa kuwa tukio la kushtusha zaidi hasa kwa wanawake katika jamii hiyo, wakijiuliza ni nini hasa kimetokea na kama hata wao wanaweza kukumbwa na hali kama hiyo kwa kuwa kuna kosa la kimila walilolifanya!


Hata hivyo, juu ya hoja hiyo, Mkurugenzi wa Shirika la Haki za Watoto Afrika Kusini la Khula Community Development Project, Petros Majola anaamini kuwa, jamii inapaswa kuelimishwa juu ya mtoto anayezaliwa katika hali hiyo ili wasije wakamdhuru.

“Jamii hii lazima ijue kwamba mama hakupenda au siyo hitaji lake mwanawe awe hivi. Kwenye tumbo la mama mjamzito hakuna kiwanda cha kujenga mtoto kinachosimamiwa na mama. Watu wanahitaji kumkumbatia huyu mama na mtoto wake na siyo kuleta imani za kishirikina au kutaka kumdhuru mtoto kwa kuona kama ni mkosi,” anasema Majola kwa vyombo vya habari.


UCHUNGU
Picha za kichanga huyo zimekuwa zikisambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii na kuwa na maoni tofautitofauti huku akina mama wakidai kuhisi uchungu na kumhurumia mama huyo kwa kubeba mimba miezi tisa akiamini atajifungua mwanawe mzuri, lakini amekutana na mtoto wa aina hiyo.Ukiacha lile la mama aliyejifungua jiwe, tukio hili linatajwa na wengi kuwa ni la kushtusha zaidi, licha ya kwamba matukio ya akina mama kujifungua viumbe wa ajabu yamesikika mno sehemu mbalimbali duniani.


TATIZO
Hadi sasa kichanga huyo yuko chini ya wataalam wa afya nchini Afrika Kusini wakimfuatilia kwa karibu.Lakini kwa mujibu wa Daktari wa Gazeti la IJUMAA WIKIENDA, Dk Abdallah Mandai, mtoto huyo alikuwa na tatizo liitwalo Progeria wakati wa uumbaji tumboni mwa mama yake.


“Hili ni tatizo ambalo humfanya mtoto kuwa na muonekano wa uzee. Hujulikana zaidi kwa jina la Hutchson Gilford Progeria.“Ni miongoni mwa magonjwa adimu zaidi ambao uwezekano wake wa kutokea ni kwa mtu mmoja miongoni mwa watu milion nane waliozaliwa.


UMRI WA KUISHI
“Huu ugojwa ni wa vinasaba (genetic) na mgonjwa wake huwa anazeeka haraka sana kuliko kawaida. Kiasi cha miaka anayoweza kuishi mtu mwenye Progeria kinakadiriwa kuwa ni miaka 12 hadi 15 ingawa kuna waliowahi kuishi hadi miaka 18. “Mbaya zaidi huu ugonjwa hauna kinga wala Tiba,” anasema daktari huyo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad