Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Mabasi yaendayo haraka (Udart), John Nguya amesema wameamua kusitisha safari za Shekilango - Mwenge na Morocco-Kawe kutokana na uhaba wa abiria na ubovu wa barabara.
Akizungumza na Mwananchi leo Septemba 9 jijini hapa, Nguya amewaondoa wasiwasi abiria wa usafiri huo kuwa kutokana na mabasi 210 waliyo nayo kwa sasa usafiri utaboreshwa kadri siku zinavyokwenda na kueleza anaamini ipo siku watu wataacha mabasi yao binafsi na kutumia usafiri huo.
Kwa upande mwingine, Nguya amesema wameanzisha safari ya kuanzia katika kituo cha mabasi cha Magufuli kwenda Kivukoni na Kituo cha Magufuli -Gerezani ili kuwapunguzia adha ya usafiri abiria wanaopanda mabasi ya mikoani.
"Tumepeleka mabasi yetu huko ili kuwapunguzia adha ya usafiri abiria wa mikoani na kuwapunguzia gharama. Kwani kuna wakati abiria hujikuta akitumia kiasi cha fedha kikubwa kuliko alichotumia kutoka mkoani, hivyo tumeliona hili, na kuamua kutatua changamoto hiyo," amesema Nguya.