Maiti iliyozuiwa Muhimbili siku sita yazikwa






Siku sita baada ya Zena Mussa Ramadhani kufariki katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Oktoba 18, 2021 na maiti yake kuzuiliwa, hatimaye jana amezikwa.
Zena amezikwa katika makaburi ya Mabrouk yaliyopo Yombo saa 12:30 jioni.

Awali, ndugu na jamaa wa marehemu Zena walikwama kuchukua mwili huo Jumatatu baada ya kutakiwa kulipa Sh1.6 milioni, zikiwa ni gharama za matibabu ambazo walidai hawakuwa na uwezo wa kulipa.

Hata hivyo, uongozi wa Muhimbili uliwataka ndugu hao kufuata utaratibu uliopo wa kupata msamaha, ikiwamo kujadiliana namna ya kulipa deni hilo, jambo ambalo wanandugu hao walishindwa wakidai kutakiwa kulipa Sh600,000 kwanza na kuacha kitambulisho, fedha ambazo hawakuwa na uwezo nazo.

Uongozi huo pia ulishatolea ufafanuzi suala hilo ukisema kuwa uliwaelekeza wanafamilia kurudi hospitalini, kama wangeshindwa kupata kiasi hicho.

Hata hivyo ndugu wa marehemu walikanusha hilo, wakidai wakidai walipewa sharti la kuwa na Sh600,000 au Sh700,000.

Mwili wa Zena ulizikwa baada ya msemaji wa familia, Ibrahim Omary kujitokeza kumalizia taratibu alizokuwa ameanza hospitalini hapo, baada ya ofisi ya ustawi wa jamii kumtaka kwenda kuchukua mwili na si mwingine

Mwili wa Zena ulikuwa hospitalini hapo kutokana na deni la Sh1.6 milioni lililotokana na matibabu, kiasi ambacho familia yake ilishindwa kulipa.

“Tunashukuru sana, leo siku ya saba, mwenzetu anaenda kupumzika,” alisema mmoja wa ndugu wa marehemu.

Wakabidhiwa mwili

Licha ya waliokuwa wakifuatilia kibali cha kupewa mwili huo kufika hospitalini ni kwa nyakati tofauti jana, saa saba mchana waliruhusiwa kuchukua mwili huo

“Waliponipigia simu mimi huku nyuma nikaanza taratibu za kufuatilia ikiwemo msikitini, malaloni na kuandaa msiba. Lakini pia kufanya taratibu za gari ya kwenda kuchukua mwili,” alisema Hadija Rashid ambaye ni mmoja wa wanandugu.

Mwananchi jana lilishuhudia shughuli za mazishi kuanzia swala ya maiti iliyofanyika baada ya Swala ya Maghrib hadi maziko ya Zena yaliyofanyika katika makaburi ya Mabrouk.

Deni lasemehewa

Zena alizikwa ikiwa ni baada ya kusamehewa deni la matibabu walilokuwa wanadaiwa ambalo pia lilipunguzwa hadi kuwa kati ya Sh600,000 hadi Sh700,000.

Kwa mujibu wa Mkuu wa kitengo cha mawasiliano kwa umma wa MNH, Aminiel Aligaesha, miongozo inaelekeza ndugu wa karibu aliyeandikishwa wakati wa kuhudumia mgonjwa, ndiye anayetakiwa kupewa mwili wa marehemu.

“Na kama yeye hana uwezekano wa kufika, anatakiwa kuandika barua ya kumtambulisha mtu mwingine kuwa ndiyo apewe mwili,’’ alisema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad