Wasanii mahiri wa kike ambao pia wamekuwa katika ushindani kimuziki Rubi na Nandy leo wataonesha kuwa wanawake wakiwa na lao wanaungana.
Tamasha hilo linaloenzi nia ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza Michezo ni la kwanza hapa nchini kwa wanawake kucheza michezo wao wenyewe.
Baada ya miaka mingi ya kukwepana na kila mmoja kuonekana anapania kufanya vizuri zaidi ya mwenzake leo Jumamosi, Septemba 18, 2021, Tamasha la Michezo ya Wanawake la Tanzanite linawakutanisha kwenye Uwanja wa Uhuru hapa Dar es Salaam.
Michezo mingi leo ikiwa ni siku ya tatu tayari imeanza asubuhi na itaendelea hadi jioni ambapo saa kumi jioni Simba Queen itaoneshana ubabe na Timu ya Taifa ya Wanawake U23 kwenye Uwanja huo wa Uhuru.
“Wasanii zaidi ya 10 watakaopanda stejini leo wakiwemo Nandy na Rubi watu wajazane uwanjani kabla ya saa nane kwani baada ya hapo kutakuwa na ufunguzi na wasanii hawa watatumbuiza mpaka jioni,” ametangaza MC wa sherehe hizo jana jioni wakati wa mapambano ya ndodi uwanjani hapo.
Wasanii wengine wakali wa kike wanaotarajiwa kuwepo leo (wakisindikizwa na kaka yao mkali wa Singeli Sholo Mwamba) ni Angela wa Konde Gang, Linnah, Lulu Diva, Malkia Hadija Kopa, Shilole, mkali wa hip hop Rosaree na wengine wengi.