Je unalifahamu jengo la Burj Khalifa lililoko Dubai? Burj Khalifa ni jengo refu zaidi duniani linalodhihirisha uwezo mkubwa wa wahandisi majengo wa karne ya 21. Unapozungumzia urefu wake au kutazama muundo wake, kwa hakika jengo hili litakushangaza; jengo hili liligharimu takriban dola bilioni 1.5 za Kimarekani kulijenga. Pamoja na kuwa ni jengo refu zaidi duniani, jengo hili limevunja rekodi nyingine kadha wa kadha zilizokuwa zimewekwa na majengo mengine.
Naamini unapenda kulifahamu zaidi ili kuongeza maarifa yako. Karibu ufuatilie makala hii ili nikujulishe mambo 20 usiyoyajua kuhusu jengo hili la Burj Khalifa.
1. Burj Khalifa ni jengo refu zaidi lililotengenezwa na binadamu duniani, lina urefu wa futi 2,723 au mita 829.8 kutoka kwenye kilele chake hadi ardhini. Hivyo kulifanya jengo hili kuwa refu zaidi huko Dubai, Umoja wa falme za Kiarabu, Mashariki ya Kati na Duniani. Jengo hili ni refu mara 3 kuliko mnara wa Eiffel huko Ufaransa na mara mbili zaidi kuliko Dola State Building.
2. Jengo hili awali lilikusudiwa kuitwa Burj Dubai, lakini baadaye likaitwa Burj Khalifa kumuenzi Sheik Khalifa bin Zayed al-Nahayan aliyekuwa kiongozi wa falme za Kiarabu.
3. Eneo lake la kutazamia mandhari (observatory deck) liko kwenye muinuko wa futi 1483 au mita 452.1 kutoka chini. Hili ni eneo ambalo watu husimama na kutazama mji au mazingira kwa chini. Hii ni kusema kuwa eneo hili liko kwenye mwinuko wa umbali wa takriban urefu wa viwanja vinne na nusu vya mpira wa miguu.
4. Jengo hili lina ghorofa 163 zilizoko juu ya uso wa ardhi na moja iliyoko chini ya uso wa ardhi.
5. Ujenzi wa jengo hili ulipendekezwa mwaka 2003, likaanza kujengwa mwaka 2004 na kisha kukamilika mnamo mwaka 2010.
6. Jengo hili limeshikilia rekodi mbalimbali za dunia kama vile “jengo refu zaidi duniani”, “jengo lenye lifti inayosafiri kwa kasi na kwa urefu mkubwa zaidi”, “eneo la kutazamia lililoko juu zaidi (observatory deck)” na “jengo linalokaliwa na watu wengi zaidi”. Hata hivyo rekodi ya eneo la kutazamia lililoko juu zaidi imeshachukuliwa na jengo la Canton Tower lililofunguliwa mwaka 2011.
7. Jumla ya kiasi cha alminium zilizotumika katika jengo hili zina uzito wa takriban sawa na ndege ya Airbus ya 5 A380.
8. Zege iliyotumika kujenga jengo hili inakadiriwa kuwa na uzani wa takriban sawa na tembo laki moja (tembo mmoja ana uzito wa wastani wa Kilo 5,443).
9. Wakati wa siku za kukamilisha jengo, takriban wafanyakazi 12,000 walihusika kufanya kazi kila siku.
10. Iligharimu takriban saa milioni 22 ya binadamu ili kukamilisha kazi hii ya ujenzi wa jengo la Burj Khalfa.
11. Nondo zilizotumika katika kujenga jengo hili ni nyingi kiasi cha kutosha kukamilisha robo moja ya kuizunguka dunia (Tani 55,000).
12. Vioo takriban 26,000 vilitumika kufunika eneo la nje la jengo hili. Wataalamu wa kufanya kazii hii kutoka China wapatao 300 walihusika kuweka vioo hivi.
13.Jengo hili linahitaji lita za maji zipatazo 250,000 kila siku. Pia jengo hili hutumia umeme mwingi ambao ungetosha kuwasha balbu 360,000 za volti miamoja kwa wakati mmoja.
14. Lifti za jengo hili zimetengenezwa kwa namna ya kipekee ambayo itawaruhusu watu kujiokoa wakati wa hatari kama vile moto au uvamizi.
15. Kuna mashine takriban 12 za tani 13 zilizojengwa nje ya jengo hili ambazo hutumiwa kufanyia usafi vioo vya jengo hili.
16. Muundo wa jengo hili umeiga umbo la ua la Hymenocallis ambalo lina vitu kama bomba vinavyorefuka katikati ya mmea wake.
17. Jengo hili lina ngazi 2,909 zinazokwenda hadi ghorofa ya 160.
18. Inasadikiwa kuwa jengo la Burj Khalifa ni jengo lililopigwa picha zaidi duniani.
19. Kutokana na urefu wa jengo hili, linaweza kuonekana hadi umbali wa kilometa 95 toka lilipo.
20. Jengo hili lina makumbusho ya picha yenye kazi za wasanii zaidi ya 85. Pia jengo hili lina funguo takriban 4,500 zinazotumiwa na watu wa usalama.
Hitimisho
Ni wazi kuwa binadamu amepewa uwezo mkubwa sana wa kufanya mambo mazuri na ya kushangaza. Naamini kupitia makala hii umejifunza mengi hasa kuhusu jengo la Burj Khalifa ambalo ni jengo refu zaidi duniani.