RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amegusia janga la UVIKO-19, mabadiliko ya tabia nchi na swala la usawa wa kijinsia katika hotuba yake ya kwanza kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linalo keti katika mkutano wake wa 76 jijini New York nchini Marekani.
Rais Samia amesema Tanzania kama nchi nyingine duniani zimeathirika na uwepo wa UVIKO-19 na kuzitaka nchi tajiri duniani kusaidia mataifa yanayoendelea kupata ziada ya chajo pamoja na kuwezeshwa kutengeneze chanjo za kukabiliana na virusi hivyo hatari.
Kwa mujibu wa Rais Samia wakati mataifa mengi yanayoendelea yakiwa yametoa chanjo kwa watu chini ya asilimia mbili, mataifa tajiri ulimwenguni yameanza kutoa chanjo ya tatu. Kutokana na kutokuwa na usawa Rais Samia ametahadharisha kuwa, “hakuna atakaye kuwa salama hadi sote tutakapo kuwa salama.”
Vilevile Rais Samia amesema serikali yake hutumia asilimia 2 hadi 3 ya mapato ghafi kugharamia shughuri za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi. Amezitaka nchi zilizo endelea kutimiza ahadi waliyotoa ya kuchangia walau Dola za Marekani bilioni 100 kwa mwaka kutekeleza makubaliano ya Paris.
Kuhusu usawa wa kijinsia, Rais Samia ambaye ni Mwanamke wa Kwanza Tanzania kukalia kiti cha Urais amekiri anamzigo mkubwa wakuwezesha usawa wa kijinsia
“Serikali yangu inakagua mifumo ya sera na sheria ili kuweka mipango itakayoweza kutekelezeka na inayoweza kupimika ili kuhakikisha uwezeshaji wanawake kiuchumi lakini pia mambo mengine yanayohusu usawa wa kijinsia,” amesema Rais Samia.