Dada wawili wa Kijapani wamethibitishwa na kitabu cha rekodi za dunia cha Guinness World Record kama mapacha wazee zaidi wanaofanana duniani kwa zaidi ya miaka 107 na siku 300.
Umeno Sumiyama na Koume Kodama wamevunja rekodi iliyowekwa na dada mapacha wa Japani Kin Narita na Gin Kanie.
Umeno na Koume, wote waliofafanuliwa kama watu wenye kupenda kutangamana na wengine, walizaliwa mnamo Novemba 5, 1913 kwenye kisiwa cha Shodoshima. Tangazo hilo lilitolewa Jumatatu kwendana na ‘Siku ya Wazee’ – likizo ya kitaifa huko Japani.
Kwasababu ya hali ya sasa na Covid-19, na kama tahadhari, akina dada hao – ambao wanaishi katika sehemu tofauti za Japani – walitumiwa vyeti vyao rasmi kuwasilishwa na wafanyikazi katika nyumba zao tofauti za utunzaji.
Wamiliki wa rekodi za awali Kin na Gin walikuwa wameshikilia jina la mapacha wazee zaidi duniani wanaofanana katika kipindi cha miaka 107 na siku 175 tangu kifo cha Kin mnamo Januari 2000.
Gin alifariki dunia mwaka uliofuata, akiwa na miaka 108. Mapacha hao marehemu, ambao majina yao yanamaanisha dhahabu na fedha kwa Kijapani, walikuwa wamezaliwa Agosti mosi, 1892 huko Nagoya, na walikuwa watu mashuhuri kwa vyombo vya habari katika kipindi cha muongo wao wa mwisho.
Familia ya Umeno na Koume walisema kwamba dada wote wawili walikuwa wamefanya utani juu ya kufikia umri wao. Japani, matarajio ya maisha ni ya juu zaidi ulimwenguni, na watu wazee wanapewa heshima kubwa. Mtu mzima mkongwe aliyerekodiwa, kulingana na kitabu cha Guinness, ni mwanamke wa Kijapani mwenye umri wa miaka 118 Kane Tanaka.