OFISI ya Rais -Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imetahadharisha dhidi ya matapeli wanaotumia jina la ofisi hiyo kujipatia fedha kutoka kwa watumishi wa umma na wananchi wengine.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Utumishi na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa, alitoa tahadhari hiyo jijini Dar es Salaam jana, akibainisha kuwa matapeli hao wamekuwa wakijitambulisha kuwa wanatoka Ofisi ya Mfuko wa Utumishi wa Umma.
Akizungumzia kuibuka kwa wimbi hilo la utapeli kwa watumishi wa umma Mchengerwa alisema uchunguzi wao umebaini watu wanaofanya vitendo hivyo sio watumishi wa umma bali ni matapeli.
"Hawa watu wamekuwa wakiwapigia simu baadhi ya watumishi wa umma wakiwaomba pesa ili wawasaidie watumishi hao kwenye mambo mengi kama vile upandishaji vyeo, uteuzi, kulipwa malimbikizo ya madai yao, uhamisho, ulipaji mafao na uhakiki wa vyeti.
"Hawa matapeli wamekuwa wakiwapigia simu watumishi wa umma na kuwaambia watume pesa ili waweze kutatuliwa changamoto hizo.
"Kibaya zaidi wengine wamekuwa wakilaghai watumishi kwa kutumia jina Mheshimiwa Rais, waziri au maofisa mbalimbali waliopo katika Ofisi ya Rais - Utumishi wa Umma," alionya.
Mchengerwa alisema serikali ipo macho na inaendelea kuwasaka matapeli hao, akionya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.Alisema watumishi wa umma na wananchi wengine wanapawa kutambua kwamba serikali ina taratibu zake inapotaka kupeleka taarifa kwa watumishi wa umma, hivyo watumishi wanapaswa kuwa makini.
Waziri Mchengerwa aliwataka watu wote wanaojihusha na vitendo hivyo vya udanganyifu, kuachana navyo mara moja kwa kuwa Ofisi ya Rais - Utumishi wa Umma kwa kushirikiana na vyombo vingine vya kiserikali wanawasaka wahalifu hao.
"Niwaombe Watanzania ukipigiwa simu na tapeli akajitambulisha kwa mfumo ambao tumeueleza hapo, toa taarifa kwangu na makatibu wakuu."Hiyo namba ya huyo tapeli aliyokupigia simu unaweza ukaitolea taarifa Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kwa kuituma namba hiyo kwenda namba 15040.
"Mtumishi yeyote yule wa umma anayetaka kuwasilisha malalamiko yake serikalini, atatumia namba 02621660240 na hapo atawasiliana na sisi moja kwa moja," alisema.
*Imeandaliwa na Edwin Mosha (TUDARCo), Irene Mwakatobe (TUDARCo) na Halfani Chusi