MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amewakana washtakiwa wenzake watatu waliokuwa makomando wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Kikosi 92 KJ leo katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, akiwa chini ya ulinzi wa askari Magereza, baada ya kuwasili katika Mahakama Kuu ya Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, mkoani Dar es Salaam leo.
Licha ya kuwakana na wao kumkana, washtakiwa wote wamekana mashtaka ya kesi ya ugaidi wanayoshtakiwa ikiwamo kula njama kufanya ugaidi na kumsababishia majeraha aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya.
Hata hivyo, makomando hao wamekiri kufahamiana kwa madai walikuwa wanafanya kazi pamoja Kikosi cha Makomando Ngerengere.
Hayo yamebainika leo Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi wakati washtakiwa wakijibu mashtaka yanayowakabili na kusomewa maelezo ya awali.
Washtakiwa walijibu mashtaka mbele ya Jaji Mustapha Siyani, huku Jamhuri ikiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando, Nassoro Katuga, Ignas Mwinuka, Esther Martin na Wakili wa Serikali Tilimanyo Majigo na Jenitreza Kitali.
Upande wa utetezi unawakilishwa na Wakili Peter Kibatala, John Mallya, Jebra Kambole, Sisty Aloyce, Nashon Mkungu, Michael Mwangasa, Alex Maseba, Faraja Mangula, Dickson Matata, Evaresta Kisanga na Hadija Aron.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mbowe, makomando Halfan Bwire, Adam Kasekwa, maarufu Adamu na Mohamed Ling'wenya, ambao wanakabiliwa na mashtaka sita.