Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu wasomewa upya mashtaka yao sita mbele ya Jaji Mustapha Siyani
Mbowe na wenzake wamefikishwa katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi leo Ijumaa Septemba 10, 2021 ambapo kwa mara ya kwanza Leo wataruhusiwa na Mahakama hiyo kujibu tuhuma zinazowakabili kwa kusema ndio wanakubaliana na tuhuma au hapana hawakubaliana na tuhuma hizo.
Mbowe anashtakiwa pamoja na Halfan Bwire Hassan, Adamu Hassan Kasekwa maarufu kama Adamoo na Mohamed Abdillahi Ling’wenya ambao wote ni makomandoo waliofukuzwa kazi jeshini kutokana na sababu mbalimbali. Watuhumiwa wanakabiliwa na mashtaka sita, likiwamo la kukutwa na sare na vifaa vya Jeshi la Wananchi (JWTZ). Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Agosti mosi na Agosti 5 mwaka jana.
Vilevile wanatuhumiwa kupanga vitendo vya kigaidi ambavyo ni kulipua vituo vya mafuta na maeneo ya mikusanyiko na kumdhuru aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya.