Mbunge wa Singida Magharibi Elibariki Kingu amesema ameshangazwa na Chama chake ambacho ni Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kutomchukulia hatua mwanachama wake na mbunge wa Kawe Askofu Josephat Gwajima kutokana na kauli anazotoa.
Kingu ameeleza hayo leo Agosti 31, 2021 wakati akichangia hoja iliyowasilishwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge juu ya mashauri mawili dhidi ya wabunge Askofu Josephat Gwajima wa Jimbo la Kawe na Jerry Silaa mbunge wa Ukonga.
''Hata Halima Mdee aliyekuwa mbunge wa Kawe hajawahi kutufanyia vitimbi vya namna hii anavyofufanyia Askofu Gwajima hili jambo limetufedhesha na mimi nimeshangaa chama changu kwanini kimekaa kimya hakija chukua hatua,'' amesema Elibariki Kingu.
Aidha, ameongeza kuwa, ''Kwa mujibu wa uchambuzi wangu Askofu Josephat Gwajima alidhamiria kuichonganisha serikali ya Rais Samia na wananchi ili watu waache kuwa na imani na serikali kwa kitendo chake cha kusema chanzo hii haijafanyiwa utafiti mkiitumia italeta madhara''.