KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida mwanamke mmoja, Regina Frednand (46) mkazi wa Mtaa wa Butiama Kata ya Sima katika Halmashuari ya Mji wa Bariadi amezua taharuki baada ya kudai kuwa amejifungua mnyama aina ya Kalunguyeye.
Jambo hilo limezua hofu na taharuki kubwa kwa wakazi wa mji wa Bariadi, baada ya mama huyo kudai kuwa amejifungua mnyama huyo badala ya binadamu kama ambAvyo imezoeleka.
Akiongea na waandishi wa habari waliofika nyumbani kwake na kukuta umati wa watu ambao walifika kushuhudia tukio hilo, mama huyo amesema kuwa tukio hilo lilitokea Jumapili ya Septemba 12, 2021.
Regina amesema kuwa, majira ya saa 1:10 asubuhi wakati akijiandaa kwenda kwenye ibada ya kwanza kanisani, ghafla alijisikia maumivu makali tumboni na ndipo akaelekea chooni kujisaidia haja ya kawaida.
“Baada ya kufika chooni huku nikiwa na maumivu makali, haja ambayo nilikuwa nikisia haikutoka… cha kushangaza nilisikia maumivu makali sehemu za siri na kuhisi kuna kitu kinaning’ata.
“Kadri maumivu yalivyoongezeka nikajisikia kusukuma ndipo kikatoka kitu ambacho sikukielewa…nikapiga kelele kuomba msaada kwa watoto wangu ambao naishi nao hapa, baada ya kufika walikitazama na kubaini kuwa alikuwa panya buku, baadaye wakakimwagia maji ya baraka ndipo kilipogeuka na kuwa mnyama aina ya Kalunguyeye,” ameeleza Regina.
Hata hiyo, alipouliza kama alikuwa mjamzito, Regina alikiri kweli kuwa alikuwa na ujauzito wa miezi mitano ambao aliupima mwenyewe nyumbani kwa kutumia kipimo cha mkono alichonunua duka la dawa.
Hata hivyo, Regina mbali na kudai kuwa alikuwa na ujauzito, lakini hakuwahi kwenda kliniki kwa madai kuwa alikuwa anasubiri ujauzito ufikishe miezi sita ndipo tukio hilo lilitokea kabla ya kuanza kliniki.
“Baada ya tukio kutokea nikawaita ndugu na wazazi wangu waje kushuhudia tukio ambalo lilikuwa la ajabu, siku ya Jumatatu yake nilijisikia vibaya nikaamua kwenda hopsitali ya Wilaya Somanda kwa ajili ya vipimo.
“Nilifika hospitali nikawaeleza tukio zima, kisha nikafanyiwa kipimo cha mionzi (Utlrasound) na majibu ya kipimo hicho yalionyesha hapakuwa na kitu chochote tumboni,”amesema Regina.
Mwanamke huyo amesema kuwa, baada ya kutoka hospitali wameendelea na maombi nyumbani hapo huku wakiwashirikisha viongozi wa dini ambapo myama huyo alichomwa moto na viongozi wa dini.
Majirani na ndugu
Mama mzazi Regina Maimuna Fransic amesema kuwa, baada ya kupigiwa simu na mtoto wake alifika nyumbani hapo na kukiri kweli kuwa alikuta amejifungua mnyama huyo na kubaki wanastaajabu.
“Kila mtu hapo ndani tulibaki tunashangaa hili jambo limetoka wapi, katika historia ya ukoo wetu halijawahi kutokea, mtoto wangu na mme wake wamekuwa wakiishi kwa kumtegemea Mungu,” amesema Maimuna.
Hata hivyo Mama mzazi na Regina alipoulizwa kama mtoto wake alikuwa na ugomvi na mtu, alisema kuwa hakuwahi kusikia uwepo wa jambo hilo au ndoa yake kuwahi kuingiliwa na mtu mwingine.
Naye Paul Manyangu mmoja wa majirani nyumbani hapo, alisema yeye alishirikia kumsaidia mama huyo baada ya kupiga kelele chooni, ambapo walishangaa kuona amejifungua mnyama.
“ Tulibaki kila mtu na mshangao na kuogopa sana, lakini ndiyo hali halisi iliyojitokeza kila kitu tunamwachia Mungu yeye ndiye anajua nini kipo nyuma ya pazia, lakini kwa jinsi ambavyo tumeishi na hii familia ni watu wa kumtegemea Mungu sana,”amesema Manyangu.
Daktari.
Mganga mfadhiwi haspitali ya halmashauri ya mji wa Bariadi (Somanda), Dkt. Emmanuel Costanine alikiri mama huyo kufika hospitalini hapo na kufanyiwa vipimo ambavyo vilionyesha hakuwa na ujauzito wala hakujifungua.
Dkt.Costantine amesema kuwa, walimfanyia vipimo viwili, ambapo cha kwanza ni kipimo mkono ambacho kilionyesha hakuwa na ujauzito wowote na kipimo cha pili ni Ultrasound ambacho kilionyesha tumboni hapa kuwepo na kitu chochote na wala hakujifungua.
Polisi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, ACP Richard Abwao alikiri jeshi hilo kupokea taarifa za tukio hilo, ambapo wanaendelea na uchunguzi zaidi ili kubaini ukweli wake ikiwemo kupata taarifa za kitaalamu kutoka kwa madaktari.
Na Derick Milton, Simiyu