Kuishi kwingi kuona mengi, ndivyo unavyoweza kusema juu ya mkasa uliompata dereva wa lori, Kennedy Mkonyi ambaye alitekwa Zambia Desemba 2020 na kuishia gerezani hadi hivi sasa akisubiri hatima ya kesi inayomkabili. Dereva huyo alikuwa amebeba madini ya shaba kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) akipeleka Dar es Salam.
Mkonyi, anayefanya kazi katika Kampuni ya Diana Rose inayosafirisha mizigo, alipokwenda polisi kuripoti tukio hilo akakamatwa na kupelekwa gerezani akisubiri hatima ya kesi aliyofunguliwa.
Simulizi ya dereva huyo anayeshikiliwa katika moja ya magereza Zambia ni mfululizo wa madhila yanayowakuta madereva wa malori wawapo safarini katika nchi za Zambia na DRC, huku wamiliki wa kampuni za usafirishaji mizigo wakitajwa kuchangia.
Hata hivyo, mke wa dereva huyo, Silvia Mkonyi anadai kuwa kampuni ya Diana Rose imemtelekeza mfanyakazi wake na familia hiyo inashindwa kumudu gharama za maisha, ikiwemo kushindwa kuwalipia ada watoto wawili wanaosoma chuo.
Hata hivyo, kuhusu madai hayo ya kumtelekeza dereva wao, Meneja Ajira wa kampuni hiyo, Mashauri Mussa anasema suala hilo liko mahakamani hivyo asingependa kulizungumzia kwa kina.
“Bado kesi iko mahakamni huko Zambia kwa miezi minne sasa, lakini tumekuwa tukitoa msaada wa matibabu na chakula kwa huyo dereva kupitia wakala wetu Zambia,” anasema Mussa.
Akieleza jinsi mume wake alivyoingia kwenye janga hilo, Silvia amesema alisafiri tangu Novemba 2020 na baada ya mwezi mmoja kupita, hakukuwa na dalili ya kurudi kwa kuwa hata simu yake haikuwa ikipatikana.
“Nilipiga sana simu yake bila mafanikio na nikajaribu kupiga kwa madereva ninaowafahamu ndipo wakaniambia kuwa, mume wangu alitekwa na alipopatikana alitoa taarifa polisi lakini akapelekwa gerezani,” anasema Silvia.
Anasema alimuuliza bosi wa mume wake kinachoendelea Zambia lakini majibu aliyopewa yalimkatisha tamaa.
Balozi anena
Balozi wa Zambia nchini Tanzania, Benson Chali anasema Zambia imekuwa ikitumika kama njia tu ya kupitishia mizigo kutoka Tanzania kwenda DRC, kwa hiyo Serikali haiwezi kunyang’anya mizigo kama imekidhi vigezo na vibali vyote.
“Kumekuwa na tabia ya wasafirisha mizigo baadhi yao kusafirisha kwa magendo na Zambia ni nchi yenye maeneo ya ukaguzi, ukifika katika maeneo hayo kama huna kibali chochote cha mzigo utanyang’anywa hata hiyo shaba inayotoka DRC, nyingine zinakuwa hazina kibali, wanaosema wananyang’anywa huo ni uongo,” anasema Chali.
Kampuni, familia zavutana
Mwananchi, lilifika katika ofisi za Diana Rose zilizopo Mbezi, Dar es Salaam kuonana na uongozi wa kampuni hiyo ambao umekiri kumfahamu Mkonyi na kwamba, bado anaendelea kulipwa mshahara.
Mussa anasema kwa miezi minne sasa wamekuwa wakitoa msaada wa matibabu na chakula kwa Mkonyi kupitia wakala wa kampuni hiyo aliyepo Zambia.
Anasema pia wamekuwa wakifanya kazi na mdogo wa Mkonyi, ambaye amekuwa akipata fursa ya kusafiri kwenda DRC na ofisi ikitoa fursa kwa dereva huyo kupita katika gereza la Zambia kumjulia hali kaka yake, lakini pia ofisi imekuwa ikitoa msaada kwa familia.
“Tumekuwa tukituma mshahara kwa mke wake pamoja na mwajiriwa wetu ambaye yuko gerezani huko Zambia, licha ya kwamba gari alilokuwa nalo lilisharudishwa na linaendelea na shughuli za usafirishaji wa mizigo kama kawaida baada ya polisi na Mahakama kujiridhisha na vielelezo,” anasema Mussa.
Hata hivyo, maelezo hayo yamepingwa na mke wa dereva huyo, Silvia aliyezungumza na Mwananchi mwisho wa wiki iliyopita, akisema tangu mumewe aliposhikiliwa maisha yamekuwa magumu.
“Meneja rasilimali watu wa kampuni ya Diana Rose amekuwa akinijibu wakati wote kuwa hawahusiki na mume wangu na kwamba niende huko Zambia kumtafuta maana hata mkataba wake ulishaisha Juni 2021,” anasema Silvia mwenye watoto wanne.
Anasema watoto wawili wanaosoma vyuo lakini wameshindwa kuendelea kwa kukosa ada.
“Mtoto wangu mkubwa alikuwa mwaka wa tatu Chuo cha CDTTI Mabughai wilayani Lushoto, Tanga hajamaliza huu muhula wa mwisho na hata mitihani ameshindwa kufanya sababu ya ada. Huyu wa pili anasoma Taasisi ya Uhasibu Arusha, naye ameshindwa kufanya mitihani muhula wa pili karudishwa nyumbani, hata sielewi nifanye nini,” anasema Silvia.
Kuhusu watoto wengine wanasoma Beseli English Medium na mwingine amemaliza darasa la saba hivi karibuni. “Huyu aliye darasa la saba amefanya mtihani wa Taifa akiwa na barua ya Mahakama ambayo shule iliiandikia mahakama kutaka kufahamu mzazi wake atalipaje ada kwa mujibu wa sheria maana amesoma mwaka mzima bila kulipa ada, sijui nitaitoa wapi, familia inanielemea naomba nisaidiwe,” anasema Silvia.
Mtoto wa kwanza, anayesoma CDTTI, Walter Mkonyi ameieleza Mwananchi kuwa, sasa anamsaidia mama yake kazi za nyumbani baada ya kurudishwa kutoka chuo kwa kukosa ada.
“Ukweli tangu baba apate matatizo tumekuwa na maisha magumu mno na sijui tutajikwamua vipi na hali hii,” anasema Walter.