SERIKALI imesema Tanzania ni miongoni mwa nchi ziliyoathirika na janga la corona, ambapo tayari kuna wagonjwa nchini na wengine wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa huo unaotikisa dunia nzima.
Hayo yamesemwa leo Jumamosi, Septemba 4, 2021 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa wakati akizungumza na wanahabari jijini Dodoma na kuongeza kuwa Serikali inawakumbusha wananchi kujikinga na janga hili, kunawa mikono, kuepuka mikusanyiko, kuvaa barakoa, kufanya mazoezi, kupata chanjo.
“Tunahimizwa wale ambao wanazidi umri wa miaka 18 kujitokeza katika vituo mbalimbali twende tukachanje kwa sababu wataalam wametuhakikishia ukichanja unajiepusha na hatari ya kifo, au kuugua sana.
“Tangu zoezi la chanjo lianze, kwa juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan tulipata dozi za kwanza 1,058,400 mpaka sasa zaidi ya Watanzania 325,000 (31.5%) wamepokea chanjo na zoezi linakwenda vizuri katika vituo mbalimbali nchi nzima.
“Chanjo ni hiari, mtu yeyote ana hiari ya kupokea chanjo ama kutokupokea, lakini wataalam wanatuambia usipopata chanjo ukaumwa, unapata madhara makubwa kwenye mwili wako. Siyo suala la kushangilia kwamba nimeumwa corona nimepona, wapo watu viungo vyao vinaathirika.
“Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan anaendelea kufanya juhudi za kupata chanjo zaidi kwa ajili ya Watanzania na yapo matumaini makubwa ya kupata chanjo baada ya shehena ya dozi 1,058,400 iliyoletwa Julai 24, 2021 kutoka Marekani kuisha.
“Serikali imetoa muda wa kati ya tarehe 01 – 07 Septemba, 2021 kwa kampuni hizi za simu kuweka sawa mitambo yao ili punguzo la asilimia 30 na asilimia 10 katika tozo za miamala ya simu lianze,” amesema Msigwa.