KWA hali ilivyo kwenye ndoa nyingi, itoshe tu kusema sasa tumefika pabaya! Ndivyo unavyoweza kusema baada kusikia kisa hiki cha kutisha kinachomhusu mama aitwaye Nancy Majonhi mwenye umri wa miaka 42.
Nancy ambaye ni mwanamke wa nchini Zimbabwe amekiri kumuua kwa kumchinja mumewe mwenye umri wa miaka 44 aitwaye Prosper Chipungare; tukio ambalo lilijiri nyumbani kwao mwaka 2015 katika Kijiji cha Ledig jimboni Sun City, Afrika Kusini walikokuwa wakiishi kabla ya mwanamke huyo kurejea kwao, Zimbambwe.
Nancy anasema kuwa, amefikia hatua ya kukiri kwa Jeshi la Polisi nchini humo baada ya kuchoshwa kuandamwa na mzimu wa mume wake huyo ambapo amekuwa hata usingizi hapati kwa miaka minne sasa.
Kwa mujibu wa Nancy alimmua mumewe huyo kwa kumpiga na nyundo kisha kumkatakata vipandevipande na kwenda kutupa maiti yake kwenye majalala matatu ya chemba za choo baada ya kutokea kutokuelewana kati yao akimtuhumu kwa matumizi mabaya ya pesa za familia.
Nancy anasema kuwa, baada ya kumuua, alijitahidi kupoteza kabisa ushahidi wote kisha kwenda Polisi kuwaambia mume wake amepotea.
Taarifa zinaeleza kwamba, Polisi walifuatilia suala hilo kwa namna zote walizojua wao, lakini hawakufanikiwa hivyo walikata tamaa.
Hata hivyo, inaelezwa kwamba, miezi kadhaa baadaye, Nancy alirudi nyumbani kwao, Zimbabwe kisha aliwajulisha ndugu zake kuwa mume huyo ambaye alikuwa mchimbaji wa madini alipotea.
Inasimuliwa na vyombo vya habari nchini Zimbabwe kwamba, licha ya kujikausha kwa muda mrefu, lakini sasa amenyoosha mikono kutokana na dhahama anayokutana nayo kutoka kwa mumewe huyo.
Nancy amewaambia Polisi na familia yake mkasa mzima ambapo mwanzo walidhani labda amepatwa na kichaa.
Hata hivyo, mwenyewe aliwaambia ni mzima wa akili isipokuwa kwa miaka minne sasa halali kwani muda mwingi mzimu wa mume wake unamuandama, unamtokea na unamwambia akakiri kumuua ndipo atapata amani.
Inaelezwa kwamba, ndugu zake wamekuwa wakishirikiana na Polisi ambapo walisafiri pamoja hadi Afrika Kusini ili Nancy akatoe ushahidi.
Wakiwa Afrika Kusini, Polisi na mtuhumiwa huyo na ndugu zake walikwenda eneo husika ambapo alionesha alipoyatupa mabaki ya mwili wa mumewe, lakini walikuta vyoo vilishabomolewa.
Polisi walichimba eneo hilo na kukuta mabaki ya binadamu ambapo DNA zilitakiwa kufanywa na kesi hiyo bado inaendelea mahakamani.
Kwa mujibu wa kaka wa Nancy aitwaye Andrew, dada yake alikiri kumuua mumewe baada ya kuwaambia kuwa alikuwa anawindwa na mzimu wake.
Kwa upande wake, mwanaume aliyewapangisha wanandoa hao nyumba mwaka 2013, Theo Sedumedi alisema alishtushwa na habari hizo kwani walihangaika wote kumtafuta mumewe bila mafanikio.
Nancy anatarajiwa kufikishwa mahakamani siku ya Septemba 21, mwaka huu akituhumiwa kwa kesi ya mauaji ya mumewe.
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako