Polisi, Msajili wabaini tatizo kisheria kuzuia vikao vya siasa



 
JESHI la Polisi nchini limekutana na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kujadili masuala mbalimbali, huku wakibainisha kuwapo kwa shida ya kisheria kwenye vikao vya ndani vya vyama vya siasa.

Kikao hicho kilifanyika jana jijini hapa ambapo Mkuu wa Jeshi hilo (IGP), Simon Sirro, alisema wamekutana kujadili vikwazo vilivyokuwa vinajitokeza kwenye baadhi ya vyama vya siasa kwenye mikutano yao ya ndani na nje ambayo wamekuwa wakizuia.

“Kimsingi tumezungumza na kuona kweli kwenye mikutano yao ya nje hakuna shida na si vyama vingi vinavyolalamika kuwa tumekuwa tunaingilia, lakini shida kubwa ipo kwenye mikutano ya ndani na tumeona upande wa sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi wasaidizi na sheria ya vyama vya siasa havijatamka bayana kuhusu sheria inayotawala vikao vya ndani vya vyama.”

“Kumekuwapo na mwingiliano au sintofahamu kwa maana kwamba baadhi ya vyama vya siasa mkutano badala ya kuufanyia nje wanakuja kuufanyia ndani na wanapofanyia ndani mikutano ya nje mara nyingi lazima tuambiwe ajenda za mkutano huo ni kitu gani… kwa changamoto hiyo inaonekana kuna ombwe la kutokuwa na sheria ambayo inayoelezea mikutano ya ndani maana yake nini na sheria inayotawala mikutano ya ndani ya namna gani,” alisema.

Alishauri Msajili wa Vyama vya Siasa kulizungumzia hilo na wanasiasa ili polisi ambao ni wasimamisizi wa sheria waone uelekeo.


 
“Lakini jambo kubwa katika mikutano yote miwili ya hadhara na ya ndani sisi Jeshi la Polisi tunaangalia usalama kwanza, tunaangalia suala la amani na utulivu katika hiyo mikutano tukiangalia suala la amani na utulivu ni changamoto au kuna tishio lolote la amani na utulivu basi ni lazima tuchukue hatua kwasababu ni kazi yetu ya msingi.”

“Lakini jingine tulichoona suala la kukata rufani kwa waziri pale ambapo OCD ametoa angalizo au amekataa kile kikao au mkutano usiendelee basi ni vizuri akawashauri viongozi wa kisiasa kuona watumie ile forum ya kuweza kukata rufani kwa waziri ili waziri aweze kubatilisha maamuzi ya OCD au kuona kwamba maamuzi ya OCD ni sahihi,” alisema.

Hata hivyo, alisema wamekubaliana kuna kila sababu ya jeshi hilo kuwa karibu na viongozi wa vyama vya siasa kwa kuwa ni wadau muhimu katika suala la ulinzi na usalama.


“Tumekubaliana mambo mengi ya kufanya kuhakikisha mwisho wa siku nchi yetu inakuwa ya amani na utulivu. Niwaombe kwa sababu msajili wana kikao cha kukutana na wanasiasa niwaombe basi ni vizuri na sisi tukapata taarifa kwa kuwa lengo ukipata taarifa unaitumia taarifa ili mwisho wa siku ni kuhakikisha kwamba nchi yetu inakuwa na amani na utulivu,” alisema.

Naye Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, alisema kikao hicho mchakato wa vikao vya awali kabla ya kufanya kikao cha wadau Oktoba 21, mwaka huu.

“Sikupenda kusubiri nifanye kikao moja kwa moja cha wadau kabla ya wahusika wakuu wa suala hili ambalo tulikuwa tunalifuatilia kukaa nao. Nashukuru tumepata ushirikiano mzuri na tumeongea mambo mengi ambayo na mimi yamenifungua macho kwamba tumekuwa tukifanya kazi lakini cha msingi nilichojifunza mawasiliano ya mara kwa mara kwenye hizi taasisi ni muhimu,” alisema.

Aliongeza: “Nitawaeleza wanasiasa mambo yaliyoelezwa, lakini kikubwa tunataka kupunguza misuguano ambayo haina ulazima… leo nimegundua kwamba kuna mambo ambayo hatuyajui sisi, lakini wangekuwa kila kitu wanakieleza tungejua tunafanya siasa au wakati mwingine tunafanya fujo, kwa hiyo tutafikisha kwa wadau wa siasa ili kuwa na mwelekeo mzuri.”

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad