Dar es Salaam. Shahidi wa tatu katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi ya uhujumu uchumi inayowakabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu, Konstebo Ricardo Msemwa ameieleza mahakama kuwa ndiye aliyewapokea washatakiwa wanaotuhumiwa pamoja na Mbowe.
Askari huyo wa Kituo cha Polisi Oysterbay, ameieleza Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kuwa alishtuka aliposikia kuwa watuhumiwa hao wanakabiliwa na kosa la ugaidi.
Alieleza kuwa kabla ya kuwapeleka mahabusu katika Kituo Kikuu cha Pollsi Dar es Salaam baada ya kuwapokea wakitokea Moshi walikokamatiwa, aliwahoji, pamoja na mambo mengine, kuhusu afya zao ambapo walimwambia zilikuwa njema.
Kesi hiyo ndogo iliibuka baada ya upande wa utetezi kupinga kupokelewa kwa maelezo ya mshtakiwa wa pili, Adamu Kasekwa, kwa madai kuwa aliteswa kabla ya kutoa maelezo na yalichukuliwa nje ya muda wa kazi kisheria.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Mustapha Siayani ni Halfan Bwire Hassan na Mohamed Ling’wenya ambao wanakabiliwa na mashtaka sita, mawili kati yake yakiwa kula njama ili kutenda vitendo vya kigaidi ambayo yanawakabiliwa washtakiwa wote wanne.
Mengine ni kufadhili vitendo vya kigaidi kwa Mbowe pekee yake na mali za kutekelezea vitendo vya ugaidi yaani silaha (bastola) kwa Ling’wenya peke yake na kukutwa na sare na vifaa vingine vya Jeshi la Wananchi (JWTZ) kwa Halfani.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga, Konstebo Ricardo alisema siku hiyo, Agosti 7 mwaka jana alikuwa anafanya kazi Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam katika chumba cha mashtaka na kwamba alikuwa na jukumu la kuwashughulikia mahabusu.
Alisema baada na wakati akikabidhiwa watuhumiwa hao kutoka wilayani Moshi walikodaiwa kupanga mikakati ya kumdhuru aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, alielezwa watu hao walituhumiwa kwa kosa la kula njama kutenda vitendo vya kigaidi katika maeneo tofauti nchini.
Alipoulizwa na Wakili Katuga kama anaweza kuwakumbuka watuhumiwa hao alijibu akiwaona anaweza.
Baada ya kumaliza ushaidi wake, shahidi huyo alifanyiwa madodoso na mawakili wa utetezi ambao walimhoji lakini alionekana kuwa imara kwani alikuwa akijibu kwa kujiamini na kutoa ufafanuzi wa kina bila kubabaika.
Shahidi aliulizwa kama mtuhumiwa mahabusu hatakiwi kutolewa bila kuridhia naye akajibu si hivyo bali anaweza kutolewa wakati wowote hata kuhamishwa na hatakiwi kugoma. Mkuu wa chumba cha mashtaka ndiye anatakiwa kuridhia kutolewa au kuhamishwa kwa mtuhumiwa aliye mahabusu.
Amri ya kumtoa mtuhumiwa mahabusu alisema inaweza kutolewa kwa maandishi au kwa mdomo na maelekezo aliyoyapata siku hiyo yalikuwa ya mdomo.
Wakili wa utetezi pia alitaka kujua iwapo mtuhumiwa akifikishwa chumba cha mashtaka (CRO) anatakiwa kupelekwa kwa daktari kwanza lakini shahidi akasema huo si utaratibu bali anaweza kupelekwa hospitali iwapo ataumwa.
“Kwanza anataarifiwa OCS (mkuu wa kituo) na yeye ndiye anafanya utaratibu wa kumpeleka mtuhumiwa hospitali,’ alisema shahidi huyo.