Polisi jijini Dodoma wanadaiwa kumfanyia vitendo vya ukatili dereva wa bodaboda kwa kumuingiza mti wa ufagio sehemu ya haja kubwa na kumsababishia majeraha.
Dereva huyo wa bodaboda ambaye pia ni mcheza muziki, Ally Bakari (21) mkazi wa Kata ya Mkonze amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, General kwa ajili ya matibabu.
Bakari alidai kufanyiwa ukatili huo kwa kupigwa, kunyofolewa rasta, kuteswa na kutobolewa utumbo kwa kuingizwa mti wa ufagio sehemu ya haja kubwa na watu aliodai ni polisi.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Onesmo Lyanga licha ya kuthibitisha kuwapo kwa tukio hilo, alisema bado haijajulikana kama waliofanya tukio hilo ni askari polisi, lakini wanaendelea kuchunguza.
Akizungumza na gazeti hili, Ally alisema Agosti 21, 2021 alitoka kwenye sherehe katika ukumbi wa Cavillum uliopo maeneo ya Kikuyu jijini hapa, kabla ya kufika nyumbani yeye na rafiki zake walikwenda baa ili kupata kinywaji, ambapo waliwakuta watu wawili, mwanamke na mwanamume wakiwa wamekaa pamoja, wao wakaagiza kinywaji.
Alisema alipoletewa kinywaji alipokuwa akikifungua alipigwa na mtu asiyemfahamu akidai kuwa alikuwa anakunywa bia yake na hicho kikawa chanzo cha ugomvi.
“Sikukubaliana na kipigo hicho, ndipo nikamshika mkono akaniambia unajivunia wenzako ngoja nikuonyeshe, wakaja watu watatu wakanifunga pingu nikahoji mbona mnanipiga kama mwizi, wakasema unaongea sana ngoja tuwaonyeshe na wenzako ndipo wenzangu wakakimbia,” alidai.
Alidai walimchukua na kumpeleka nyuma ya baa hiyo ambako walianza kumuingiza kijiti cha ufagio sehemu za haja kubwa huku wakimnyofoa rasta zake. “Wakanigeuza huku wakisema wananifanyia kitendo cha hatari na kuanza kunichomeka jiti huku nyuma, kumbe wanavyochomeka wanatoboa na utumbo, baada ya kufanya vile waliniweka katika buti la gari na kunipeleka nisikokufahamu nikiwa nimetepeta kwa kipigo na mateso yale,” alidai.
Alidai baada ya kushauriana walikubaliana wapige simu polisi na ‘difenda’ ikaja na kumchukua na wao wakapanda kwenye gari yao ndogo wakaondoka kuelekea kituo kikuu cha polisi na walipofika walimuweka mahabusu. “Nilikuwa nimepoteza fahamu, nilistushwa na makelele ya mahabusu wakisema anakufa,” alidai.
Kutokana na hali aliyokuwa nayo ya kutoa kinyesi na damu masikioni, machoni kila mtu aliogopa kumsogelea, ndipo akachukuliwa na watuhumiwa wenzake na kuwekwa nyuma ya kituo kwa amri ya polisi.
“Baada ya muda akaja askari nikamwambia mimi si mwizi na sijawahi kuiba cha mtu kwani kosa langu nini mpaka nimefika hapa, akasema unasemaje wewe mbwa, sasa ngoja tukuonyeshe akatoka na fimbo akaanza kunipiga tena,” alidai.
Kauli ya polisi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Onesmo Lyanga alisema tukio hilo bado linachunguzwa.
Akizungumzia madai ya wahusika kuhusishwa na polisi kwa kuwa walikuwa na pingu, Lyaanga alisema si sahihi kudhani kuwa Jeshi la Polisi ndio linalomiliki pingu peke yake, bali zinamilikiwa katika maeneo mbalimbali.
“Hujawahi kuona askari Magereza wamemfunga mahabusu pingu? Hivyo si kila mwenye pingu ni polisi, halafu kwa maelezo aliyoyatoa yule kijana bado tunachunguza, hatuwezi kunyooshea kidole polisi kwa sababu ya pingu, ingawa hatuwezi kuacha lipite, tunaendelea kufuatilia,” alisema Lyanga.
Kuhusu upelelezi wa tukio hilo ulipofikia, Lyanga alisema “tutakwenda eneo la tukio ambalo ni eneo la baa linalokuwa na watu wengi, sasa kwa nini wasitokee watu wakasema kwamba tuliwaona moja, mbili, tatu wakifanya moja, mbili tatu sijui, tusianze kupakazia mtu yeyote wala chombo chochote kile. Kwa sasa ni upelelezi,” alisema.
Kauli ya hospitali
Mwananchi lilimtafuta Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Ibenzi Ernest kuhusu matibabu ya Ally, lakini alimpa mwandishi wetu namba ya simu ya daktari anayemtibu kijana huyo aliyemtaja kwa jina la Dk Kato. Hata hivyo, Dk Kato alipopigiwa simu alisema yuko nje ya mji kwa majukumu mengine, huku akishauri afuatwe ofisa mawasiliano wa hospitali. Naye pia alitaka aandikiwe barua kwenda kwa mkurugenzi wa hospitali, ndipo majibu ya matakwa ya taarifa ya mgonjwa yatolewe ndani ya siku tatu.
Kauli ya mke wa Ally
Hawa Abasi, ambaye ni mke wa Ally alisema siku ya tukio mume wake alimuaga kwenda kwenye shughuli na hakurudi.
Alisema asubuhi alifuatwa na rafiki wa Ally na kupewa taarifa za kukamatwa na polisi kwa kosa la kuleta fujo baa. “Nilipofika kituoni nilimkuta mume wangu na kuna askari akaniuliza kwamba mume wangu ni shoga au teja? Nikamjibu si kweli, akasema sasa mbona kila sehemu anatoa damu nikamjibu sijajua ila hizo kazi mume wangu hafanyi, ni dansa na bodaboda,” alisema.
“Akaniambia nimuwekee dhamana, wengine wakaniambia ‘mchukue mzoga’. Mume wangu hajawahi kuwa mkorofi,” alisema.
Kauli ya mjomba wa Ally
Kwa upande wa mjomba wa Ally, Ramadhani Saidi, alisema Jumapili alipigiwa simu na rafiki wa Ally kujulishwa kuhusu kukamatwa kwake.
Alisema baada ya kutoka kwa dhamana aliyowekewa na mkewe, alipigiwa simu tena kujulishwa kuwa Ally ana hali mbaya, alipokwenda alimkuta damu zinatoka sehemu za siri na masikioni, hali iliyowalazimu kumrudisha hospitali huku wakipita polisi kwa ajili ya kupata fomu namba 3, PF3.
“Niliwaambia nina mgonjwa wangu kapigwa na anadai kapigwa na askari, tunaomba PF3 akapate huduma, yule askari alichosema hivi, yaani ukishasema kapigwa na askari huwezi kupewa PF3, itaonekana watajishtaki wenyewe. Kama unataka kumuokoa mgonjwa wako nenda hospitali, sema amepata ajali atapokelewa, tulimpeleka hospitali, kutokana na hali yake kuwa mbaya alipokelewa. Alisema baada ya kumuacha mgonjwa hospitali walirudi kituoni na wakapewa askari, alichukua maelezo ya awali ya Ally akiwa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu.