JESHI la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, limesema linawashilikia baadhi ya watu kuendelea na uchunguzi dhidi ya tukio la Hamza Hassan.
Jumatano iliyopita katika eneo la Selander, Hamza ambaye sasa ni marehemu, aliwashambulia askari kwa kuwaua wanne na kujeruhi wengine sita na yeye kuuawa.
Kamanda wa kanda hiyo, Jumanne Muliro, alipoulizwa na gazeti la Nipashe kuhusiana na uchunguzi dhidi ya ndugu wa Hamza ambao baadhi yao bado wanashikiliwa, alisema upelelezi unaendelea.
Kuhusu idadi ya wanaoendelea kushikiliwa hadi siku hiyo, kamanda Muliro alisisitiza kuwa, “upelelezi bado unaendelea.”
Kuhusu majeruhi wa tukio hilo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Aminiel Aligaesha, alisema wote waliruhusiwa Jumatatu ya wiki hii.
Hamza kabla ya kuuawa aliwashambulia askari wawili waliokuwa kwenye kibanda maeneo hayo ya Selander kisha akachukua silaha zao mbili aina ya pistol na kuanza kurusha risasi ovyo na kusababisha vifo vingine viwili vya askari na kuwajeruhi watu sita.
Mauaji hayo yalitokea wakati Hamza akirushiana risasi na polisi karibu na Ubalozi wa Ufaransa hadi kupigwa risasi na kufa na polisi kushikilia baadhi ya ndugu zake akiwamo mama na wadogo zake kwa mahojiano, baadhi yao kuachiwa na wengine kuendelea kubaki.
Waliouawa katika tukio hilo ni askari watatu wa Jeshi la Polisi na mmoja kutoka kampuni ya ulinzi binafsi.