Raia wawili wa Canada waliofungwa China waachiwa huru





Wafanyabiashara wawili wa Canada waliokuwa wamefungwa nchini China wameachiwa huru muda mchache baada ya Canada nayo kumwachia mkurugenzi wa kampuni ya Huaweai Meng Wanzhou.
Waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau amethibitisha taarifa za kuachiwa huru raia hao wawili Michael Kovrig ambaye ni mwanadiplomasia wa zamani na mfanyabiashara Michael Spavor. Trudeau amesema ndege iliyowabeba imeondoka China na inatarajiwa kuwasili Canada leo Jumamosi.

Raia hao wawili walikamatwa na kufungwa kwa mashitaka yanayohusiana na ujasusi baada ya Canada kumkamata mkurugenzi wa kampuni ya Teknolojia ya Huawei Meng Wanzhou. Kovrig na Spavor walishitakiwa Machi mwaka huu na mnamo mwezi Agosti Spavor alihukumiwa miaka 11 jela wakati hapakuwa na uamuzi katika kesi inayomhusu Kovrig. Waziri Mkuu Trudeau awali alilaani hukumu hiyo akisema "haikubaliki na isiyo ya haki".

Mapema, jaji wa Canada alisimamisha kesi iliyokuwa inahusu kumpeleka Meng Marekani na kuondoa masharti ya dhamana,  na hivyo kumruhusu kurejea China kwa mara ya kwanza tangu kukamatwa kwake katika uwanja wa ndege wa Vancouver mwaka 2018.

Kuachiwa kwake kumetokana na makubaliano yaliyofikiwa baina ya wizara ya sheria ya Marekani, kuyasimamisha kwa muda mashitaka ya udanganyifu ambayo yalitia dosari mahusiano ya Beijing, Washington na Ottawa. Meng ambaye ni binti wa bilionea na mwanzilishi wa kampuni kubwa ya Huawei, aliachiwa mjini Vancouver, saa chache baada ya waendesha mashitaka wa Marekani kutangaza makubaliano hayo.

"Ningependa kutoa shukrani zangu kwa ubalozi wa China hapa Canada kwa kuniunga mkono", Meng aliwaeleza waandishi wa habari mjini Vancouver. Kusimamishwa kwa muda mashitaka hayo kunapunguza mvutano katika uhusiano baina ya Beijing, Washington na Ottawa wakati China ikiituhumu Marekani kwa kuishambulia kisiasa moja ya kampuni yake kubwa ya teknolojia.

Mawakili wa Meng walisema wanatarajia mashtaka hayo kufutwa ndani ya miezi miezi 14. "Tunafurahi sana kwamba wakati huu anaweza kwenda nyumbani kwa familia yake, "alisema wakili wa utetezi Michelle Levin.

Ingawa Beijing ilisisitiza wakati wote kwamba kesi hizo mbili hazikuwa zinahusiana, hata hivyo serikali ya Trudeau iliishutumu China kwa kushiriki katika diplomasia ya mateka.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad