Rais wa zamani wa Afghanistan Ashraf Ghani ameomba msamaha kwa watu wa Afghanistan baada ya kukimbilia katika nchi za Falme za Kiarabu.
“Kuondoka Kabul ulikuwa uamuzi mgumu zaidi maishani mwangu,” amesema, akiongeza kuwa anajuta kwamba “hakuweza kumaliza hilo kwa njia tofauti.”
Bwana Ghani aliondoka ghafla nchini Afghanistan wakati wanamgambo wa Taliban walipokuwa wakiendelea kuingia kwenye mji mkuu mnamo Agosti 15.
Alisema hakuwa na nia ya kuwaacha watu wake lakini “ilikuwa ndio njia pekee iliyosalia.”
Katika taarifa iliyoshirikishwa kwenye mtandao wa Twitter siku ya Jumatano, Bw. Ghani alisema hakuwa na njia nyingine yoyote zaidi ya kuondoka nchini humo ili kuepusha kuenea kwa ghasia.
“Niliondoka kwa kushawishiwa na usalama wa ikulu, ulionishauri kuwa kuendelea kuwepo kulihatarisha kutokea kwa mapigano mitaani na katika barabara za mji kama ilivyotokea wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka ya 1990,” aliandika, akiongeza kuwa alifanya hivyo “kuokoa mji wa Kabul na raia wake milioni sita”.
Alisema alikuwa amejitolea kwa kipindi cha miaka 20 kusaidia Afghanistan kuwa “nchi ya kidemokrasia, mafanikio na huru.”
Bwana Ghani ameongeza kuwa alikuwa na “masikitiko makubwa” kwamba “muda wangu mwenyewe uliishia kwa majuto kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wangu.”