Rose Mhando; Alitupwa Bongo, Kaokotwa Kenya





MWIMBA Injili Rose Mhando kwa sasa anaishi Kenya, ametunga wimbo kuwashukuru Wakenya kwa jinsi walivyookoa maisha yake.

 

Anapowashukuru Wakenya, anatoa somo kwa Watanzania kwamba, walimtupa alipokuwa hawezi, Kenya wakamuokota.

 

Rose Mhando ni mwimbaji bora wa Injili Bongo, naweza kusema ndiye aliyezaa roho za wapenda nyimbo za Injili hadi zikawa zinapigwa baa.

 

Safari yake ya kihuduma ilipoingiliwa na ibilisi, Wabongo walimtupa, hawakumjali alipougua na kudhoofika mwili. Wengi walimdhihaki kuwa anatumia madawa ya kulevya; wakampuuza.

 

Alipozushiwa kifo hakuna aliyejali kuonesha kuwa, kama kifo kingemfika wakati huo isingewauma watu kwa ukubwa wa huduma aliyotoa. Hii ndiyo tabia ambayo Wabongo waliionesha, ni wachache waliosisimama naye.

 

Cha kushangaza hata wachungaji “wazee wa maombezi” hawakutaka kuhangaika naye, badala yake akaenda kuombewa na wachungaji wa Kenya na kuhudumiwa hadi amepona na sasa anamtukuza Mungu kwa ajili yao.

 

Hapa kuna somo la kujifunza kwa wasanii; “kuwa na roho ya kuvushana kwenye matatizo.”

Wasanii hawatakiwi upeana kisogo na kuombeana mabaya, wanatakiwa kuwa jeshi la kuokoana pale mmoja wao anapoonekana kashikwa na mambo ya duniani.

 

Mfano Ray C, kama asingekuwa Rais mstaafu Jakaya Kikwete kujitolea, pengine leo angekuwa ameshapoteza maisha.

Hata sasa ni wasanii wangapi hawawezi, lakini wametelekezwa na kusemwa vibaya kutokana na pengine kutopea kwenye madawa ya kulevya au ulevi wa pombe? Wasanii wanatakiwa kukumbuka kuwa hata tembo huinuana.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad