Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuachia huru mfanyabiashara James Rugemalira ikieleza kuwa mkurugenzi wa mashtaka nchini Tanzania (DPP) hana nia ya kuendelea na kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa mahakamani hapo tangu Juni, 2017.
Mbali na Rugemarila, mshatakiwa mwingine katika kesi hiyo ni mwanasheria wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Joseph Makandege na wote walikuwa wakikabiliwa na makosa ya kughushi, kutakatisha fedha na kuongoza genge la uhalifu na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Wakili wa Serikali mwandamizi, Grace Mwanga amedai kuwa upande wa mashtaka hawana nia ya kuendelea na shauri hilo kupitia kifungu cha 91(1) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya mwaka 2019.
"Hatuna nia ya kuendelea na kesi hii, tunaiomba mahakama hii imwachilie huru mshatakiwa Rugemalira," amesema Mwanga.
Baada ya maelezo hayo Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi alikubali ombi lililotolewa na upande wa jamhuri na kumuachia Rugemalira.
"Kesi naiahirisha hadi Desemba 23, 2021 na mshtakiwa Makandege ataendelea kuwa mahabusu,” amesema hakimu huyo.