Serikali kuita mashahidi saba kesi ndogo ndani ya kesi ya kina Mbowe


Serikali imesema kuwa itakuwa na jumla ya mashahidi saba katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu.

Mbowe na wenzake wanakabiliwa na kesi ya Uhujumu Uchumi, wakituhumiwa kujihusisha na makosa ya Ugaidi.

Kesi hiyo namba 16 ya mwaka 2021 inayosikilizwa na Jaii Mustapha Siyani katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, imeanza kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashtaka leo Jumatano Septemba 15, 2021, huku Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni (RPC) Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Ramadhani Kingai akifungua pazia la ushahidi wa upande wa mashtaka.

Hata hivyo Mahakama imelazimika kusimamisha usikilizwaji wa kesi hiyo badala yake sasa inasikikiza kesi ndogo kuhusiana na maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa pili, Adamu Kasekwa baada ya upande wa utetezi kuyapinga yasipokewe mahakamani kama sehemu ya kielelezo  cha ushahidi wa upande wa mashtaka.

Kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Peter Kibatala amedai kuwa maelezo hayo yalichukuliwa zaidi ya saa mbili na kwamba pia yalitolewa baada ya mshtakiwa kuteswa.

 Kutokana na hali hiyo kama ilivyo kawaida Mahakama imelazimika kuendesha kesi ndogo ili kujiridhisha kama kweli maelezo hayo yalichukuliwa nje ya muda wa kisheria na kama alilazimishwa.

Wakili wa Serikali, Robert Kidando ameieleza Mahakama kuwa watakuwa shahidi saba na kwamba leo wanaye shahidi mmoja, ambaye ni Kingai ambaye anaendelea na ushahidi.

Kwa hiyo mpaka Mahakama itakapomaliza kusikiliza mashahidi hao wa Jamhuri kisha wa utetezi kisha itatoa uamuzi wa kuyakubali au kuyakataa ndipo kesi ya msingi itakapoendelea ambapo ACP Kingai ataendelea na kesi ya msingi.

Mbali na Mbowe na Adamu, washtakiwa wengine ni Halfan Bwire Hassan na Mohamed Ling'wenya.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad