KATIKA sehemu ya kwanza jana, kuliainishwa madai yaliyopo kuhusu walakini wa upelelezi kisheria na mazingira yake.
Endelea kufuatilia uchambuzi wa hoja hiyo, ikioanishwa na nafasi zingine za kisheria zinazogusa kasoro hiyo:
Katika hoja yake, Mwanasheria Alloyce Komba anafungamana na kinachopaziwa sauti na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), akianzia na eneo la upelelezi ambalo anawasilisha hoja yake ya msingi kwamba: "Tunataka upelelezi wa kesi zote za Uhujumu Uchumi na kesi zingine uwe na ukomo."
Anaendelea: "Hii itapunguza mwenendo wa watu kushikiliwa mahabusu kwa muda mrefu kwa kisingizio kwamba upelelezi haujakamilika."
Komba pia anadai madaraka ya DPP yamepitiliza, hivyo yanapaswa kupunguzwa ili kuondoa mianya anayodai inaweka rehani sehemu ya haki za kibinadamu.
Anafafanua kwamba DPP anachukua nguvu ya mahakama, akirejea mifano hai ya kesi za Uhujumu Uchumi zinazotakiwa kusikilizwa na Mahakama Kuu, lakini zinapokuwa makahama za wilaya au mkoa zinahitaji kibali chake.
Mwanasheria huyo mwenye mzizi wa kutumikia Sekta ya Habari na sasa wakili wa kujitegemea, anafafanuzi kwamba mashtaka ya jinai hayapaswi kukinzana na Katiba ya nchi.
Hata hivyo, katika maoni yake ya kitaalamu huku akirejea baadhi ya vifungu vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, anadai mwenendo wa kesi iliyomhusu Rugemalira ulikiuka sheria hiyo kuu.
Wakili Benedict Ishabakaki ana dai la kukosoa taratibu za upelelezi nchini, akitaka ufanyike mapema na hatua za kujiridhisha zifikiwe na mamlaka za kisheria, ndipo shauri lihamie kwenye utaratibu wa kufikishwa mahakamani.
Huku akitoa mfano anaoueleza katika sura ya walakini unaoshuhudiwa kwenye shauri linalomhusu Mzee Rugemalira, wakili huyo anafafanua:
"Mtu akikamatwa wakati ushahidi haujakamilika, matatizo yake ndiyo kama haya yaliyotokea kwa Rugemalira, mtu anakaa mahabusu miaka minne ila hamna kitu chochote walichokikuta kwenye kesi yake."
KAULI YA SERIKALI
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Geofrey Pinda, alipotakiwa na Nipashe kutoa neno kuhusiana na sauti hizo kutoka kwa wanasheria wenzake, kwanza alikiri ukweli unaolalamikiwa wa kilio cha kesi kuchelewa mahakamani.
Hata hivyo, anasogeza kando lawama za kuchelewesha kesi kwa wadau wenza kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Ofisi ya Rais (Utawala Bora) penye mzizi wa mashauri.
Pinda anafafanua: "Kesi ni jambo mtambuka, kuna TAKUKURU, Polisi, wote hao ni wapelelezi. Wakitoka hao anaingia DPP, yeye anajiridhisha kama kesi inastahili kusikilizwa mahakamani na kama ina maslahi makubwa zaidi, Wakili Mkuu wa Serikali anaingia.
"Hivi vyote vinafanyiwa kazi kila kimoja kwa wakati wake na tukumbuke kesi zinatofautiana uzito. Unaposema kuchelewa kwa kesi, lazima ujue kwanza sura ya kesi husika.
"Mahakama katika sura ya kawaida inaonekana kama ndiko mahali kesi zinakocheleweshwa, lakini ukweli ni kwamba mahakama haihusiki na upelelezi.
"Jaji au hakimu akiambiwa upelelezi umekamilika, anapanga tarehe ya kusikiliza ushahidi na baadaye hukumu. Tumejitahidi sana kupunguza msongamano wa kesi, mkakati wetu ni mzuri na kesi sasa zinakwenda kwa haraka."
Anasema hatua inayochukuliwa hivi sasa, wamepeana wito kwa wizara na vitengo vyote wadau wa kesi kuharakisha hatua za upelelezi kukiwapo muda maalum.
"Tumeweka malengo kesi za kawaida uchunguzi usizidi siku 60 na hizi kesi kubwa usizidi miezi sita. Tumejitahidi sana kuhakikisha kesi zinaamuliwa haraka," anafafanua hatua inayochukuliwa, akiwa na angalizo kuwa mashauri makubwa upelelezi unaweza kuvuka ukomo.
Nini kilichojiri kisheria kwenye shauri linalolalamikiwa sasa linalomhusu Rugemalira na wenzake? Ni swali ambalo Nipashe inataka ufafanuzi kutoka kwa kiongozi huyo wa serikali.
Naibu Waziri katika majibu yake, anaeleza: "Kesi ya Rugemalira iliangukia kwenye Uhujumu Uchumi na mazingira ya uhujumu yanachukua muda mrefu kufanya utafiti wa kujiridhisha.
"Hawa walifika hadi hatua ya kukubaliana na DPP kulipa. Sasa inawezekana pande zote mbili zilikuwa zinavutana kwenye hilo."
Pinda ambaye katika majibu yake kwa Nipashe, yanavaa sura tatu; nafasi ya kiutawala, uanasheria na mwananchi wa kawaida, anaungana moja kwa moja na walalamikaji wanasheria wenzake na umma kuhusu madhara ya mtu kukaa muda mrefu mahabusu.
Akitumia mfano rejea wa mshtakiwa Rugemalira, Naibu Waziri huyo anaweka ujumbe wa simanzi yake binafsi, akisema kilichomfika Rugemalira na kwa namna hiyo akiwanyoshea kidole wote waliokaa muda mrefu mahabusu katika mazingira yanayofanana na hayo, hayana jema hata kidogo.
Ni darasa la kisosholojia analozama nalo, akisema laiti inapomwangukia mwenye umri wa ujana, si ajabu pakashuhudiwa mabadiliko makubwa kwa hali ya kifamilia aliyoiacha nyumbani, tukio litakalombebesha simanzi mpya ya kijamii hadi kiuchumi, ambayo matokeo yake ni kitendawili.
Hata hivyo, udadisi wa Nipashe kuhusu madaraka ya DPP, Pinda anarejea katika nafasi yake ya kisheria, akiukosoa mtazamo wa wanasheria wenzake kuwa ni ushauri uliokosa mbadala thabiti.
Anahoji: "Mamlaka ya DPP yapunguzwe, yapelekwe wapi? Kipande cha mamlaka yale kiende kwa nani? Polisi au TAKUKURU? Hayo ni mamlaka ambayo tumempa kisheria!"
WAFUNGWA, MAHABUSI
Rais Samia Suluhu Hassan alipozungumza katika ufunguzi wa kikao kazi cha maofisa Jeshi la Polisi mkoani Dar es Salam tarehe 25, mwezi uliopita, pia alitoa angalizo binafsi, akiona ukakasi wa ziada ya mahabusi katika mazingira yanayokosa hoja nzito.
Katika hilo, Rais alitoa maelekezo kadhaa ya kuondoa tatizo hilo, ikiwamo Jeshi la Polisi kuona namna ya kukaa na wadau wake wa sheria, kuangalia uwezekano wa kurekebisha sheria inayohusu mahabusi.
Rais alikemea ucheleweshaji upelelezi unavyoibebesha mzigo mkubwa serikali kuwahudumia watu walioko mahabusu kwa muda mrefu.
Katika hotuba hiyo ya Rais iliyobeba angalizo la kitaalamu, aliainisha takwimu hadi tarehe 23 ya mwezi uliopita, kulikuwapo mahabusi 15,194 huku wafungwa wakiwa 16,542, hali inayokaribia kufanana.
"Mahabusi hawa wapo waliokaa wiki, miaka miwili, miaka mitatu, mwaka mmoja na muda mbalimbali na wanalishwa na serikali," Rais Samia alisema na kuhimiza kesi zenye ushahidi dhaifu zinapaswa kufutwa na kuwarejeshea watuhumiwa uhuru wao.