Serikali Yapiga Marufuku Walevi, Makahaba Kuchangia Damu




SERIKALI ya Uganda kupitia Bodi ya Kuchangia Damu (UBTS), imesema kuanzia sasa haitawaruhusu walevi, makahaba na watu wenye mpenzi zaidi ya mmoja kuchangia damu kwa hiyari.

 

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Benki ya Damu ya Nakasero, Samuel Wante wakati akizungumza na Gazeti la Daily Monitor nchini humo na kueleza kuwa sababu kubwa ya kukataa damu kutoka kwenye makundi hayo ya wachangiaji, ni hasara ambayo serikali imekuwa ikiingia.

 

Amesema utafiti wa kitaalamu umebaini kwamba damu inayochangiwa na walevi, makahaba na watu wenye mpenzi zaidi ya mmoja, asilimia kubwa hukutwa na maambukizi ya magonjwa kama Ukimwi, Kaswende, Kisonono na magonjwa mengine ya zinaa pamoja na yale yanayoambukizwa kwa njia ya ngono zembe.

 

Ameongeza kuwa, gharama ya kuhifadhi damu hiyo, huwa ni kubwa ambapo mwisho hubainika kwamba haiwezi kutumika na hivyo kumwagwa, wakati tayari serikali inakuwa imeshaingia gharama katika kuitunza na kuisafirisha mpaka maabara kubwa kwa ajili ya vipimo.



Wante ameongeza kuwa, kwa wale waliokuwa wakijihusisha na vitendo vya ukahaba, wanatakiwa kukaa miaka kumi tangu walipoacha vitendo hivyo ndipo waruhusiwe kuendelea kuchangia damu.

 

Alipoulizwa kuhusu watu waliopo kwenye ndoa za mitaala za zaidi ya mke mmoja kama nao wanaruhusiwa kuchangia damu, Wante amesema utafiti unaonesha kwamba watu waliopo kwenye ndoa za wake wengi, huwa ni waaminifu na hawashiriki hovyo vitendo vya kimapenzi tofauti na wake au waume zao, hivyo wao wanaruhusiwa kuchangia damu bila tatizo.

 

Mtaalamu huyo amewaasa watu kuachana na vitendo vya ngono zembe, ukahaba na ulevi, ili wawe na sifa ya kuendelea kuchangia damu akibainisha kwamba zipo faida nyingi ambazo mtu anaweza kuzipata kwa kuchangia damu.

 

Akizitaja faida hizo, Wante amesema ni pamoja na kupunguza uwezekano wa damu kuganda, kupunguza uwezekano wa kupata saratani, kupunguza shinikizo la juu la damu pamoja na kumfanya mtu kuwa na maisha marefu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad