Shahidi wa kwanza wa upande wa utetezi katika kesi ndogo inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu amedai Agosti 5,2020 akiwa na mshtakiwa wa tatu Mohamed Abdillahi Ling'wenya eneo la Rau alivamiwa na kuwekewa dawa za kulevya na bastola.
Kesi hiyo ndogo ilikuja baada ya mawakili wa upande wa utetezi kupinga maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, Adamu Kasekwa, yasipokelewe mahakamani hapo kama kielelezo.
Akiongozwa na Wakili wa utetezi John Mallya leo Septemba 24, 2021 mbele ya Jaji Mustapha Siyani shahidi huyo Adamu Kasekwa, amedai kuwa baada ya kuvamiwa na kundi hilo lenye watu zaidi ya watano walianza kumpiga.
Amedai kuwa baada ya kuwekewa vitu hivyo, watu hao walianza kusema ana dawa za kulevya na silaha ndipo mshitakiwa wa tatu alipotoa vitu vyake na yeye asiwekewe.
"Niliweza kuwatambua watu wawili Ramadhani Kingai (aliyekuwa shahidi wa kwanza) na Mkaguzi wa Jeshi la Polisi, Mahita Omary Mahita (aliyekuwa shahidi wa pili), ambao nilikuja kuwatambua hapa mahakamani," amedai Kasekwa.
Shahidi huyo ambaye alikuwa ni Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWT) kikosi cha 92 KJ Sangasanga Morogoro kwa miaka sita amedai kuwa hakuacha jeshi bali aliachishwa na mwajiri wake kutokana na tatizo la kiafya.
" Kazi iliyohusisha jeshi ni kazi inayohusu majukumu makubwa, nilihudhuria operesheni yakulinda amani Congo nilipo toka huko wakubwa waligundua nina tatizo la battle confusion, sijui nilipataje ila ni kitu ambacho humpata askari yoyote kutokana na milio ya risasi au mizinga," amedai shahidi huyo.
Akizungumzia uhusianao wake na mshtakiwa wa nne Freeman Mbowe, shahidi huyo amedai anamfahamu kwa muda mfupi baada ya kuhitajika kwenda kufanya kazi ya ulinzi kwake.
Amedai walikuwa kwenye mazungumzo ya awali ya kujaza mkataba wa kazi ukihusisha malipo na majukumu watakaokuwa nayo.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 16/2021 ni Halfan Bwire Hassan, Adamu Hassan Kasekwa na Mohamed Abdillahi Ling'wenya