PRESHA kubwa kwa sasa ni kuelekea mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya Simba na Yanga unaotarajiwa kuchezwa Jumamosi ya Septemba 25, Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kutokana na watani hawa kuwa kwenye vita ya kusaka ushindi.
Mashabiki wanahitaji kuona matokeo chanya kwa timu zao, na mshindi ni yule ambaye atafanya maandalizi mazuri kwa wakati huu. Ipo wazi kwamba utakuwa ni mchezo wenye ushindani mkubwa kwa timu zote mbili.
Jambo la msingi kuelekea kwenye mchezo huo kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ni kuangalia namna gani mashabiki wanaweza kuwa salama pamoja na mazingira ya Uwanja wa Mkapa.
Uzuri ni kwamba kila mmoja anaweza kupata ushindi na ile ambayo itashindwa kujiandaa haitaweza kupata ushindi kwani kila kitu ni maandalizi.
Kikubwa ambacho kinahitajika kwa mashabiki ambao watajitokeza Uwanja wa Mkapa ni kuacha kubeba matokeo uwanjani, na kuendelea kufanya maandalizi yao kwa hesabu ili kupata ushindi.
Kila timu inapaswa kupambana ili kupata kile ambacho kinastahili, kwa kuwa jambo la msingi ni kila mchezaji kutimiza jukumu lake uwanjani.
Mashabiki ambao watabeba matokeo mkononi huwa inakuwa ngumu kwao kuamini kile ambacho watakiona baada ya dk 90 kukamilika, hivyo jambo la msingi ni kujiandaa na kusubiri matokeo ya uwanjani.
Zile tambo ambazo kila mmoja anatamba kwa sasa acha ziendelee, lakini dakika 90 zitaamua na matokeo yatapatikana bila ubishi.
Imani yangu ni kwamba kwa sasa kila timu inahitaji kusepa na Ngao ya Jamii, hasa ukizingatia kwamba hawa ni Watani wa Jadi na kila mmoja anatafuta ile hali ya kuweza kutamba mtaani.
Mbali na kutamba pia kila timu inahitaji kuonyesha kwa mashabiki wao kwamba kweli wanastahili kutwaa Ngao ya Jamii, haitakuwa kazi nyepesi kwa timu zote mbili.
Nidhamu inahitajika kwa timu zote mbili kuanzia kwa viongozi mpaka wachezaji, waache kabisa tabia ya kuwa na matokeo mfukoni wala mkononi hii mechi haina mwenyewe.
Ikumbukwe kwamba kila timu inahitaji ushindi na hakuna timu ambayo haifikirii kuhusu kupata ushindi, lakini hakuna ushindi bila ya maandalizi mazuri pamoja na nidhamu nje na ndani ya uwanja.
Mashabiki pia ni muhimu kuelewa kwamba hakuna haja ya kuwa na presha kubwa wakati huu kila kitu ni suala la muda tu, wajitokeze kwa wingi uwanjani wakijua kwamba lolote linaweza kutokea.
Ninawasisitizia pia wachezaji wacheze kwa akili kubwa, na kuacha tabia zile za ugomvi na kutumia nguvu kwenye kusaka ushindi kwa sababu kila mchezaji anapaswa kuwa mlinzi wa mwingine.
Kwa utulivu kabisa na umakini inabidi kila kitu kiende kama ambavyo kimepwangwa, ikiwa muda huu mchezaji ataumia itakuwa ni hasara kwake na timu kwani msimu mpya huu hapa.
MOHAMMED HUSSEIN