WATU sita wakiwemo watumishi wa Serikali wilayani Mvomero wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuhusika na njama za kuvujisha mtihani wa Taifa wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Kambala iliyopo wilayani humo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Muslimu alizungumza hayo katika mkutano na waandishi wa habari juu ya opereshani iliyofanyika ya kwa siku 20 kuanzia Augosti 28, hadi Septemba 16, mwaka huu ya kupambana na uhalifu kwenye Wilaya za Mkoa huo.
Alisema watu hao baadhi yao ni walimu wa shule za msingi na Sekondari katika Wilaya ya Mvomero na wanaendelea kuwa chini ya upelelezi.
“Mtakumbuka hivi karibuni kulifanyika mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi kitaifa nchini kote ambayo ilifanyika kuanzia Septemba 8, 2021 hadi Septemba 9, 2021” alisema Muslimu.
Alisema licha ya kushikiliwa kwa watumishi hao, mtihani huo ulifanyika kwa usalama, amani na utulivu mkoani Morogoro kutokana na ulinzi mkali uliofanywa na Polisi na kwa kushirikiana na kamati ya usimamizi wa mitihani hiyo.
Aliwataja wanaoshikiliwa na baadhi ya majina yao ambao wapo kchini ya upelelezi ni pamoja na Mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Kambala, Juliana Nyumayo (40) ,mkazi wa Kambala , wilayani Mvomero.
Wengine ni Msimamizi mkuu wa Mtihani , Antonia Pastory (32) ambaye ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Doma na mkazi wa Doma wilayani Mvomero pamoja na Msimamzi mkondo C, Francis Kondo (46), mwalimu wa Shule ya Msingi Kinda , wilayani Mvomero na mkazi wa Mkundi wilaya ya Morogoro.
“Upelelezi unaendelea kwa watuhumiwa sita katika shule ya Msingi Kambala kuhusika na njama hizo “ alisema Muslimu.