SPIKA wa Bunge, Job Ndugai ameeleza kushtushwa kupitishwa kwa sheria inayomtaka mkulipa kulima ushuru wa bidhaa wa asilimia mbili kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakati Kamati ya Bunge ya Bajeti ilikataa.
Akijibu swali la Mbunge wa Namtumbo (CCM), Vita Kawawa aliyetaka kujua kama ni kweli wakulima wa tumbaku watatozwa kodi hiyo, Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema kwamba ni kweli bunge lilipitisha sheria ya ushuru wa bidhaa wa asilimia mbili kwenye mazao ya kilimo.
Hata hivyo, amesema wizara haijaanza kukata ushuru huo kwa sababu mjengeko wa bei ya tumbaku huamuliwa kati ya Februari na Aprili, na kwamba wakati sheria inapitishwa, bei ilikuwa imepangwa. Ameongeza kwamba wamewasiliana na wizara ya fedha kuona namna wanavyoweza kutekeleza sheria hiyo ila kwa kulinda maslahi ya wakulima.
Baada ya majibu hayo Spika Ndugai alitishia kuifumua Kamati ya Bunge ya Bajeti, huku akihoji wanawezaje kupitisha kitu kama hicho. Hata hivyo, mwenyekiti wa kamati hiyo, Baran Sillo alisema walilikataa jambo hilo, na hata taarifa yao bungeni, walipinga mpango huo.
Amesema kamati inapopinga jambo, lakini serikali ikaendelea kuling’ang’ania huwa ni majanga kwa wananchi. Aidha, amesema endapo kamati yoyote itakutana na hali kama hiyo tena, itoe taarifa bungeni ili bunge liwe upande wa kamati na waziri husika abaki mwenyewe