“HAPO ulipo unafanya nini? Sijui mpenzi we umeshakula. Napata shauku ya kukuona kwani tangu nilipoondoka, nataka nirudi nyumbani, nikupe stori fulani.
Tukiwa pamoja mezani, iii kwanza nipigie, mpenzi nipigie (nakupigia honey). Nipigie (oh), laazizi nipigie (Mi’ na kazi jikoni). Nipigie (Oh), wife nipigie. (Nakupigia, darling). Nipigie (Oh), honey nipigie…
Mi’ na we kitu kimoja (oh kimoja). Mi na we lengo ni moja (oh moja). Mi na we kitu kimoja (oh moja). Mi na we lengo ni moja (uh uu). Nipigie, mpenzi nipigie (Nakupigia, honey). Nipigie (oh), laazizi nipigie (Mi nakazi jikoni).
Nipigie (oh), wife nipigie (Nakupigia, darling). Nipigie (oh), honey nipigie…
Sema mpenzi unasemaje? Ndiyo naweka msosi mezani, ila nyumbani usichelewe. Mi na hamu na hiyo stori. Stori yenyewe ya nani? Usije nizuga mezani. Maana ninavyotamani (uuw).
Nipigie, mpenzi nipigie (Nakupigia, honey). Nipigie, laazizi nipigie (Naweka vocha mammy). Nipigie, oh sweetie nipigie (Ngoja niende dukani).
Nipigie, mume wangu nipigie (Ngoja niende dukani). Mi na we kitu kimoja (Mi na we kitu kimoja). Mi na we lengo ni moja (Mi na we lengo ni moja) Mi na we kitu kimoja (Najua, najua) Mi na we lengo ni moja.
(Mi na we lengo ni moja) Nipigie, mpenzi nipigie. Nipigie, mpenzi nipigie Nipigie, laazizi nipigie Nipigie, mume wangu nipigie…”
Hii ni sehemu ya mashairi matamu ya muda wote ya Ngoma ya Nipigie kutoka kwenye moja ya kolabo bora kabisa za Bongo Fleva ya Stara Thomas na AT.
Stara anatajwa kuwa mmoja wa mfano bora wa kizazi cha wanawake kunako muziki wa Bongo Fleva. Atabaki kuwa mwimbaji bora wa RnB, Soul na Zouk nchini Tanzania.
Stara ni mwenyeji wa Kanda ya Ziwa (Mwanza). Alianza kuimba akiwa na umri wa miaka saba tu! Alipokuwa sekondari alikuwa akifanya maonesho jukwaani kabla ya kujichanganya kwenye makundi ya The Kilimanjaro Band na In Africa Band.
Mbali na Ngoma ya Nipigie, Stara amesikika mno na nyimbo kibao kama Mimi na Wewe, Nyuma Sitarudi, Nipo kwa Ajili Yako, Sitaki, Ukimwi Unaua, Nashindwa, Nani Mshamba, Shoga Yangu, Niambie, na Hadithi kabla ya kujikita kwenye Gospo na kuachia Tupendane na nyingine kibao.
Usisahau, mwaka 2003, Stara alitwaa Tuzo ya Mwimbaji Bora wa Kike Tanzania kupitia Kilimanjaro Music Awards.
IJUMAA SHOWBIZ imekaa mezani na Stara ambaye anafunguka mengi kuhusu muziki;
IJUMAA SHOWBIZ: Kwanza kabisa waeleze mashabiki wako kwa nini umeacha Bongo Fleva na kuingia kwenye Injili?
STARA: Nimeamua kufanya hivyo kama yalivyo maamuzi mengine, lakini jambo la msingi sana ni kwamba nimeingia kwenye muziki wa Injili kwa kuwa nimeamua kueneza Injili kwa njia hii ya nyimbo ili nami nimtukuze Mungu.
IJUMAA SHOWBIZ: Nini tofauti katika kazi yenu ya kuimba kati ya nyimbo za Injili na Bongo Fleva?
STARA: Tofauti ipo na kwa kweli haikuwa kazi rahisi. Muziki wa Injili ni mzuri japokuwa nimekaa sana kwenye Bongo Fleva. Ukweli ni kwamba muziki wa Injili nilikuwa siufahamu vizuri.
IJUMAA SHOWBIZ: Je, ni kweli kwamba mastaa wa muziki wa Injili walikutenga au kukukataa?
STARA: Ni kweli jambo hilo lilinikumba, lakini siwezi kuwalaumu sana kwa kuwa ni moja ya changamoto za kazI. Unajua mambo haya yana vitu vingi vingine siwezi kuvisema, kifupi niseme tu kwamba ndani ya muziki wa Injili nilikutana na changamoto kadhaa.
IJUMAA SHOWBIZ: Je, wasanii wa muziki wa Injili walikuamini ulipoingia upande huo?
STARA: Kwa kweli waimbaji wa Injili hushirikiana wao kwa wao kwa kuwa wameokoka, kwa hiyo akitokea mtu kutoka upande wa pili, hawamuamini haraka kwa kuwa wanamuona hajaokoka, hivyo wanamuangalia kuona kama kweli ameamua kuingia kwenye Injili? Wanapenda kuona hata miondoko yako imebadilika.
IJUMAA SHOWBIZ: Kwenye Bongo Fleva ulikuwa unafanya kolabo, je, kulikuwa na tatizo?
STARA: Hapana, kwenye Bongo Fleva kulikuwa hakuna shida ya kolabo au kushirikiana kwani ni jambo la kawaida na halina mjadala kuliko huku ambako hakujawa sawasawa.
IJUMAA SHOWBIZ: Unawaambia nini waimbaji wa Injili kwa kuwa wewe umeshajiingiza huko?
STARA: Nawakumbusha tu waimbaji wa Injili kwamba wasibaguane wakawaona wengine kuwa wenye dhambi kuliko wao, kwa kusema kweli kama watafanya hivyo watakuwa hawatendi haki kabisa. Msanii wa Bongo Fleva akiingia kwenye Injili wampe ushirikiano kwani kwa kufanya hivyo watajenga umoja na mshikamano kwa kuwa lengo la waimbaji wa Injili ni kueneza neno la Mungu kupitia uimbaji.
IJUMAA SHOWBIZ: Unalionaje soko la Injili baada ya kuingia huko?
STARA: Kuna tofauti kubwa na soko la Bongo Fleva hasa kutokana na ujumbe unaokuwa kwenye nyimbo japokuwa zote zinalenga jamii. Muziki wa Injili una cha zaidi kwa sababu hueneza neno la Mungu wakati Bongo Fleva hutoa tu burudani na kuimba mambo ya dunia hasa mapenzi. Bongo Fleva hulenga zaidi biashara ili kuingiza mapato wakati muziki wa Injili hulenga kuitangaza Injili.
IJUMAA SHOWBIZ: Unauonaje muziki wa Injili kwa Tanzania, unasonga mbele au unarudi nyuma?
STARA: Kwa Tanzania kusema kweli muziki wa Injili unakua sana, tena kwa kasi kubwa.
IJUMAA SHOWBIZ: Kwa nini unadhani muziki wa Injili unakua kwa kasi nchini?
STARA: Unakua kutokana na wanamuziki wa Injili kutoa video zenye ubora mkubwa au niseme za hali ya juu zinazoendana na soko la kimataifa. Hivyo nionavyo mimi ni kwamba tunakoelekea ni kuzuri zaidi na tutaleta ushindani wa kimataifa.
IJUMAA SHOWBIZ: Unawaambiaje waimbaji wa Injili au wadau wake?
STARA: Ninawaambia tu kwamba waendelee kutunga nyimbo zenye ujumbe mzito wa Kibiblia na niwaombe wadau wa muziki wa Injili wawekeze zaidi kama wenzetu wa nje wanavyofanya ambao wameanza zamani kuwekeza, nasi tukifanya hivyo tutafika mbali na tutawapita.
IJUMAA SHOWBIZ: Sasa umejipangaje kuhakikisha unapaa katika muziki huo wa Injili?
STARA: Kwa sasa naweka mambo sawa ili niweze kutoa nyimbo zangu mpya ili zitoke kwa ubora wa hali ya juu na kiwango cha juu.
IJUMAA SHOWBIZ: Kwani Stara hadi sasa una albam ngapi za muziki wa Injili tangu uingie upande huo?
STARA: Mpaka sasa nina albam moja, inaitwa Nani Mshamba na ina nyimbo kumi, hii ni kwa sababu nimezoea kutoa nyimbo kumi nilipokuwa ninaimba Bongo Fleva. Sasa hivi naandaa albam ya pili.
IJUMAA SHOWBIZ: Hiyo albam ya pili unatarajia kuizindua lini na wapi?
STARA: Mpaka sasa sina uhakika lini nitaizindua na wapi, lakini ipo katika hatua ya mwisho kwenye kuiandaa studio.
IJUMAA SHOWBIZ: Utawashirikisha waimbaji gani wa Injili hapa nchini au nje ya nchi?
STARA: Nitawashirikisha waimbaji mbalimbali, lakini bado nafikiria nimuombe nani nifanye naye kazi, muda ukifika kila kitu nitaweka wazi.