Msemaji wa kundi la Taliban kwenye mji wa Kunduz ulio kaskazini mwa Afghanistan leo ameitolea wito jumuiya ya kimataifa kuharakisha utoaji wa misaada kwa nchi hiyo akisema wanamgambo hao wa Kiislamu siyo magaidi.
Akizungumza na shirika la habari la Ujerumani, dpa, Matiullah Ruhani amesema msaada huo unaweza kutolewa kwa njia ya uwekezaji, miradi ya ujenzi au msaada mwingine wowote wa kiutu kwa serikali au raia wa Afghanistan.
Ruhani pia amesema inashangaza kwamba kwa zaidi ya miaka 20, jumuiya ya kimataifa iliiunga mkono serikali iliyoangushwa nchini Afghanistan, lakini inasitasita kutoa msaada tangu Taliban ilipochukua udhibiti wa nchi hiyo.
Matamshi ya afisa huyo yanakuja katika wakati mataifa mengi duniani yanatafakari njia bora ya kuisaidia Afghanistan inayoongozwa na Taliban, kundi ambalo lina rikodi dhaifu ya kuheshimu haki za binadamu.