Tundu Lissu Ataja Haya Baada ya DPP kumfutia kesi




Dar es Salaam. Baada ya Serikali kusema haina nia ya kuendelea na kesi inayomkabili makamu mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, mwenyewe ameibuka na kuitaka Serikali kuzifuta kesi zote anazoshtakiwa pamoja na zinazowakabili wanachama wa chama hicho bila masharti akisisitiza kuzingatiwa kwa demokrasia na haki za binadamu.

Kauli ya Lissu anayeishi Ubelgiji imekuja muda mfupi baada Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumfutia kesi ya uchochezi iliyokuwa inamkabili yeye na wenzake watatu.Kesi hiyo imefutwa baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) kuieleza mahakama kuwa hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya washtakiwa hao.

Lissu na wenzake walikuwa wanakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya mwaka 2002.

Mbali na Lissu, washtakiwa wengine katika kesi ambao nao wamefutiwa mashtaka na kuachiwa huru ni Jabir Idris, mhariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina na mchapishaji wa kampuni ya Jamana, Ismail Mehboo.


Washtakiwa hao wamefutiwa mashtaka yao chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) .

Uamuzi wa kuwafutia kesi hiyo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Joseph Luambano baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya washtakiwa wote wa tuhuma zilizokuwepo.

Wakili wa Serikali, Ashura Mzava aliieleza mahakama hiyo kuwa kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kuendelea na ushahidi lakini Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) hana nia ya kuendelea nayo.


Baada ya Mzava kueleza hayo, Hakimu Luambano alisema kupitia kifungu hicho, mahakama imewafutia mashtaka washtakiwa wanne na kuwaachia huru.

Akiandika katika ukurasa wa Twitter, Lissu alisema kesi hiyo ni miongoni mwa sita zilizokuwa zikimkabili na kuna kesi za viongozi wenzake wa chama, na wanachama alizotaka zifutwe pia.

Mbali na ujumbe huo, alipotafutwa kupitia namba yake ya WhatsApp, Lissu alisema pamoja na kufutwa kesi hiyo, bado hana imani ya kurudi nchini.

“Kesi zote za uongo dhidi yangu na viongozi na wanachama wetu zifutwe bila masharti yoyote. Nihakikishiwe usalama na uhuru wangu na wote waliokimbia nchi kwa kuhofia usalama na uhuru wao. Serikali iheshimu haki za binadamu na za kisiasa na iache kuzuia mikutano inayoruhusiwa kisheria. Yote haya hayajafanyika kwa hiyo kuzungumzia kurudi nyumbani bado ni mapema sana,” alisema Lissu.


Lissu na wenzake walikuwa wakikabiliwa na mashitaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya mwaka 2002.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad