UNALINYAKA jarida la People? Yes, People Magazine. Ni jarida adhimu kwenye himaya ya Joe Biden. Lina nyota nyingi Marekani. Lina tuzo kadhaa kama jarida bora la mwaka katika nchi ya majimbo 50.
Kwa wastani, huchapwa nakala milioni 4 kwa wiki na kwa mwaka, hupata kadirio la wasomaji milioni 50. Mapato yake ni dola bilioni 1.5, yaani Sh3.5 trilioni kwa mwaka.
Sasa, jarida hilo, exclusively, jana, Septemba 7, 2021, lilichapisha picha za supastaa aliyeikacha Bongo Fleva, Vanessa Mdee ‘V-Money' na kitumbo chake. Akiwa beneti na Mr right wake, Olurotimi Akinosho ‘Rotimi'.
Habari hiyo, ilidakwa pia na vyombo mbalimbali vya habari Marekani na Ulaya, likiwemo gazeti la Daily Mail la UK. Na kwa kuwa People ndio walinunua haki ya kuunadi ujauzito wa V-Money katika nyakati zake za mwisho kuelekea kujifungua, kila chombo kilichoripoti kilitoa credit kwa People.
Nakala ngumu ya Daily Mail, husomwa na watu milioni 2.2 kwa siku, wakati mtandao wake hutembelewa na watu milioni 218 kwa siku. Kwa ukokotoaji, V-Money na kitumbo chake, ameingia kwenye mzunguko wa watu milioni 50 wa People, vilevile milioni 218 wa Daily Mail.
Na kila aliporipotiwa, utambulisho ni kuwa mwanamuziki wa Tanzania, Vanessa Mdee, anatarajiwa kupata mtoto wa kiume na muigizaji wa Power na Coming 2 America, Rotimi.
Yes, Rotimi yumo ndani ya Coming 2 America, mzigo wa 2021. Rotimi anatumia jina la Idi Izzi, mtoto wa General Izzi. Halafu huyo General Izzi ni supastaa Wesley Snipes. Galacha Eddie Murphy, yupo kama kawa! Rotimi pia yumo ndani ya series ya Power, yenye vichwa vikubwa vingi akiwemo 50 Cent.
Rotimi pia ni mwanamuziki. Hata hivyo, uhusika wake kwenye filamu ndio una nguvu kubwa Marekani.
Jinsi jina la Tanzania lilivyotajwa, maana yake nchi imetangazwa pakubwa kupitia habari ya ujauzito wa V-Money na Rotimi. Wajukuu wa Nyerere badala ya kufurahia taifa lao lilivyotangazwa duniani, wao wanahoji mbona Jux hakumpa V-Money mimba? Ni Bongo na Wabongo!
Ndimi Luqman MALOTO