STAA wa muziki nchini Marekani, Rihanna ametupilia mbali kesi dhidi ya baba yake, wiki chache kabla ya siku waliopaswa kukutana mahakamani.
Nyota huyo wa muziki aina ya pop alikuwa amemshtaki baba yake, Ronald Fenty, kwa kutumia jina lake vibaya kunufaisha kampuni yake ya burudani, na alimshtaki mnamo mwaka 2019 kwa matangazo ya uwongo na kuingilia maisha yake kwa hali iliyokiuka haki zake za kuwa na siri.
Alisema pia kwamba alijaribu kumsajili katika safari yake ya nje ya nchi bila ruhusa. Kesi hiyo ilitakiwa kuanza kusikilizwa mnamo Septemba 22, lakini Rihanna aliwasilisha ombi la kuitupilia mbali kesi hiyo Jumanne.
Hakuna sababu iliyotolewa, lakini ripoti za vyombo vya habari vya Marekani zinaonyesha kwamba walifikia makubaliano ya kutatua mzozo wao nje ya mahakama na baba yake na mwenza wake wa kibiashara.
Rihanna, ambaye jina lake kamili ni Robyn Rihanna Fenty, alifungua kesi miaka miwili iliyopita, akisema: “Ingawa Bwana Fenty ni baba wa Rihanna, hana, na hajawahi kuwa na mamlaka ya kuchukua hatua kwa niaba ya Rihanna.”
Alidai kuwa mnamo mwaka 2017, baba yake na mtu mwingine, Moses Perkins, waliunda kampuni inayoitwa Fenty Entertainment, ambayo ilidai mara kwa mara kuwa inahusiana na Rihanna.
Katika nyaraka za mahakamani, mawakili wake walisema: “Bwana Fenty na Bwana Perkins wametumia uwongo huu katika juhudi za kulaghai mamilioni ya madola kutoka kwa watu wengine kwa mabadilishano ya ahadi za uwongo kwamba wameidhinishwa kuchukua hatua kwa niaba ya Rihanna.”
Walidai kuwa kampuni ya Fenty Entertainment ilijaribu kusajili safari ya tarehe 15 Marekani Kusini yenye thamani ya $ 15m (£ 11m), na vile vile maonyesho huko Los Angeles na Las Vegas, bila Rihanna kujua.
Kwa kuongezea, walidai kwamba Ronald Fenty alikuwa akijaribu kufaidika na utambulisho wa nembo ya kibiashara ya “Fenty”, ambayo Rihanna ameitumia kwa biashara zake kadhaa ikiwa ni pamoja na ile ya vipodozi ya mamilioni ya fedha, Fenty Beauty.
Baba yake hapo awali alijaribu kuanzisha nembo yake ya kibiashara kwa kutumia jina Fenty, kama sehemu ya mpango wa kufungua msururu wa hoteli ambazo mtu pia anaweza kufanya manunuzi, alidai. Hata hivyo, ofisi inayosimamia hataza na nembo za kibiashara Marekani ilikataa ombi hilo.
Akiomba kutolewa kwa agizo la kumzuia baba yake na mwenzi wake wa kibiashara kuchukua hatua hiyo, Rihanna alisema shughuli zake za biashara zilikiuka matangazo, ushindani na sheria za faragha na pia kulihatarisha “jeraha kubwa lisiloweza kutibiwa” kwa kmpuni ya Fenty ikiwa hatua hiyo haitasimamishwa.
Mwimbaji huyo, ambaye ni miongoni mwa wanamuziki tajiri duniani, kwa muda mrefu amekuwa na uhusiano mbaya na baba yake, ambaye awali, aliwahi kupambana na uraibu wa pombe na dawa za kulevya. Hakuna kati ya wawili hao aliyepatikana mara moja kutoa maoni yake juu ya kutupiliwa mbali kwa kesi hiyo ya kisheria