Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. mwigulu Nchermba amesema kumekuwepo na baadhi ya watu kutumia fursa ya uhuru wao kupinga kila kitu ikiwemo masuala makubwa ya kitaifa jambo ambalo si afya kwa mustakabali wa taifa leo.
Mwigulu amesema hayo leo Jumanne, Septemba 14, 2021 wakati wa hafla ya uzinduzi wa kampeni ya uelimishaji na uhamasishaji kuhusu sensa ya mwaka 2022 inayofanyika katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
“Kumekuwepo na mila potofu, na wengine kukosa uzalendo kwenye masuala ya kitaifa, hata wakati wa uanzishwaji wa vijiji vya ujamaa kurahisisha maendeleo kwa jamii, wapo waliopinga.
“Hata zilipokuja chanjo za polio, Hepatitis B, polio, TB na nyingine wapo walipinga, ulipokuja uhamasishaji wa vyandarua kujikinga na malaria wapo watu walipinga, walichukua vyandarua na kufugia kuku ama kutegea dagaa.
“Hata suala la chanjo ya corona wapo waliobaki baridi na wengine wamejitokeza na kupinga, hata masuala ya sensa wapo wenye imani potofu, watapinga tu, tunataka tutumie fursa hii kupeana elimu na kuhamasishana, kila mmoja ajitokeze kuunga mkono zoezi hili ili twende vizuri.
“Mhe. Rais umeelekeza kwa vile mpango wa maendeleo wa 2025 unakaribia kuisha, tuandae mpango mwingine ambao utakuwa unazaa mipango mingine midogo midogo, tayari kazi hiyo imeshaanza.” – Dkt. Mwigulu Nchemba.