UPO uwezekano mkubwa wa kuwepo mabadiliko katika safu ya ulinzi ya Yanga katika mchezo wa marudiano wa hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United ya nchini Nigeria.
Yanga inayonolewa na Mtunisia, wikiendi iliyopita ilichezea kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Rivers mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar.
Timu hizo zinatarajiwa kucheza mchezo wa marudiano Jumapili hii huko Nigeria ambao Yanga wanahitaji ushindi wa mabao 2-0 ili wasonge katika nafasi inayofuatia ya michuano hiyo mikubwa Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, benchi la ufundi na wachezaji wa Yanga walifanya kikao mara baada ya mchezo dhidi ya Rivers sambamba kuangalia marudio ya mechi kwa ajili ya kuangalia upungufu.
Mtoa taarifa huyo alisema benchi hilo la ufundi lilibaini upungufu kadhaa ikiwemo safu ya ulinzi ambayo ilionekana kufanya makosa yaliyosababisha kuruhusu bao hilo hivyo Litombo Bangala huenda akamchomoa mmoja mechi ijayo na yeye kuanza.
Aliongeza, pongezi nyingi zilienda kwa kipa wa timu hiyo raia wa Mali, Djigui Diarra ambaye aliokoa hatari kadhaa golini kwake kama angekosa umakini, basi angeruhusu zaidi ya bao moja.
“Upo uwezekano mkubwa wa kuwepo mabadiliko katika safu ya ulinzi ikiwemo safu ya kati na huenda Litombo (Bangala) akaanza katika kikosi cha kwanza kama siyo beki wa kati basi kiungo mkabaji atakayewasaidia mabeki kupunguza na kuokoa hatari golini.
Kocha Nabi hataki kuona hilo likijirudia katika mchezo wa marudiano ya kuchukua maamuzi ya kuibadili ya safu ya ulinzi ikiwemo ya kushoto aliyokuwa anacheza Adeyum (Saleh) kwa kumtoa na kumuingiza mwingine,” alisema mtoa taarifa huyo.
Akizungumzia hilo Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela alisema kuwa: “Hilo jukumu la kocha Nabi ambaye ndiye anayejua ubora na ubovu wa kikosi chake, sisi uongozi yupo katika utawala.”
Wilbert Molandi, Dar es Salaam