Zimbabwe imewazuwia wafanyakazi wa umma ambao hawajanjwa kwenda kazini, agizo hilo likitekelezwa mara moja.
Waziri wa habari wa nchi hiyo Monica Mutsvangwa amesema kuwa serikali ilikuwa imewapatia wafanyakazi wake "muda wa kutosha " kupata chanjo za Covid-19.
Maafisa wanasema takriban 90% ya watu waliolazwa hospitalini wenye maradhi ya Covid ni wale ambao hawakupokea chanjo.
Nchi hiyo ina wastani wa wagonjwa 145 wapya wa corona kila siku na imeripoti vifo saba Jumanne kutokana na ugonjwa huo.
Karibu Wazimbabwe milioni mbili, sawa na takriban 12% ya watu wa nchi hiyo kwa ujumla kwa sasa wamepata dozi kamili ya chanjo ya Covid.
Haifahamiki wazi ni wafanyakazi wangapi wa umma wameathiriwa na uamuzi huo wa baraza la mawaziri, na iwapo wataendelea kupokea mishahara au wataweza kufanya kazi nyumbani.
Serikali ni muajiri mkubwa zaidi, na agizo hilo linaweza kuathiri huduma kama vile za afya na elimu nchini humo.
Wengi wa waalimu wa shule za umma bado hawajapata chanjo ya Covid.
Baada ya maambukizi ya Covid kupungua mwezi huu, kumbi za mazoezi ya mwili, migahawa na makanisa yaliruhusiwa kufungua milango, lakini wafanyakazi walikuwa bado hawajapata chanjo kamili.
Vyama vya wafanyakazi tayari vimeyapeleka makampuni mahakamani kwa madai ya ubaguzi dhidi ya wafanyakazi ambao hawajapokea chanjo.