Waziri Mkuu Majaliwa akataa kufungua ofisi ya TANESCO Kyerwa





WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekataa kuzindua mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera kwa sababu gharama zilizotumika ni kubwa kuliko aina na idadi ya majengo yaliyopo.

“Nikiweka jiwe la msingi nitakuwa nimehalalisha majengo mengine yajengwe kwa gharama hii. Siwezi kuweka jiwe la msingi, gharama zilizotumika ni kubwa kuliko majengo yaliyopo. Simamieni ujenzi wa majengo yenu na mjenge kwa kutumia mfumo wa force account.”



Mheshimiwa Majaliwa amekataa kufungua ofisi hiyo leo (Jumatatu, Septemba 20, 2021) wakati akiwa katika katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika mkoa huo.
“Nini kilisababisha hadi kibanda kigodo cha mlinzi kikajengwa kwa shilingi milioni saba? Kina matofali mangapi kama sio ulaji nini? hii si sahihi sijaweka jiwe la msingi wala kufungua na kile kibao kilichoandikwa jina langu kiondolewe. Serikali ipo makini katika usimamizi wa miradi na haya ni maelekezo ya Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.”



Mradi wa ujenzi huo umegharimu shilingi milioni 483.42, ambapo kibanda cha mlinzi kimegharimu shilingi milioni 7.03, uzio shilingi milioni 94.2, jengo la ofisi shilingi milioni 253.8 na stoo shilingi milioni 51.55.


Waziri Mkuu amesema Serikali inajenga majengo makubwa ya vituo vya afya ambayo ni jengo la mapokezi ya wagonjwa, maabara, chumba cha upasuaji, wodi ya mama na mtoto, nyumba ya daktari, chumba cha kuhifadhia maiti, kichomea taka na korido kwa gharama ya shilingi milioni 500.
Kufuatia hatua hiyo, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa TANESCO uhakikishe katika miradi yake mingine ya ujenzi gharama zilingane na aina na idadi ya majengo.

Naye, Meneja Mwandamizi Usambazi wa TANESCO Makao Makuu, Mhandisi Nathanasias Nangali ambaye alisoma taarifa ya mradi huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, amesema mradi huo ulianza Septemba 11, 2018 na kukamilika Februari 08, 2020 kwa gharama za shilingi 483,422,328.02.

Amesema mkandarasi aliyenga mradi huo ni kampuni ya M/S RK Ivestment chini ya usimamizi wa mkandarasi mshauri TANESCO kitengo cha miliki. “TANESCO imeendelea kutumia wataalamu wake katika kusimamia na kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa ofisi zake za mikoa, wilaya na vituo vya kupoza na kusambaza umeme.”

Amesema TANESCO imeendelea kutenga fedha kwa awamu kila mwaka ili kutekeleza miradi kama hiyo ambapo katika mwaka huu inaendelea na ujenzi wa ofisi za wilaya za Buhigwe-Kigoma, Ruangwa-Lindi, Urambo-Tabora, Gairo na Malinyi-Morogoro, Nanyumbu na Tandahimba-Mtwara, Kilolo-Iringa, Rorya na Serengeti-Mara, Laela-Rukwa na Meatu-Simiyu.

Akizungumzia  huduma ya umeme inayotolewa katika wilaya hiyo amesema kati ya vijiji 99 vya wilaya hiyo vijiji 70 vinaumeme na vijiji 29 vilivyosalia vitapata huduma hiyo kupitia mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili unaoendelea kutekelezwa.

Awali, Mheshimiwa Majaliwa alitembelea na kukagua kiwanda cha kuchenjua madini ya bati (TIN) cha kampuni ya African Top Minerals kilichopo wilayani Kyerwa ambapo alitumia fursa hiyo kumuhakikishia mwekezaji huyo kwamba Serikali itaendelea kumuunga mkono.

Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Hassan Ibar alisema mradi huo uliogharimu shilingi bilioni nne unalengo la kuboresha na kukuza sekta ya madini wilayani Kyerwa na Tanzania kwa kuongeza thamani ya madini hayo katika soko la dunia, hivyo kuongeza kipato kwa wananchi.

Aliishukuru Serikali kwa jitihada zake za kutambua mchango wa madini ya bati kwa kuzindua cheti cha uhalisia cha madini hayo ambacho kimewasaidia kutambulika kimataifa na kufanya biashara yao kwa uhakika.

“Tunaishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia kwa jitihada zake za kuweka mazingira bora na wezeshi kwa wawekezaji, tutaendelea kumuunga mkono.”

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad